KUTOKA VITA, AFCON 2025 NA KUWEKA MATUMAINI YA SUDAN
Mchezaji wa timu ya soka ya taifa ya Sudan, Ammar Taifour, amesimulia jinsi alivyonusurika mwanzo wa vita vya kikatili nchini humo, vita ambavyo Umoja wa Mataifa umevitaja kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani. Taifour, mwenye umri wa miaka 28 na uraia wa Marekani na Sudan, alikuwa katika hoteli mjini Omdurman wakati milio ya risasi iliposikika nje. Awali aliipuuza akidhani siyo hatari, lakini saa chache baadaye, watu wenye silaha walizingira hoteli hiyo wakifyatua risasi.
Taifour, pamoja na wachezaji wenzake, makocha na wahudumu wa afya, walikwama ndani ya hoteli hiyo kwa zaidi ya siku mbili huku chakula na maji vikipungua. Walifanikiwa kuondoka baada ya wapiganaji kuondoka, na Taifour akarudi Marekani, akiacha nyuma taaluma yake ya soka nchini Sudan ili kutafuta timu mpya.
Uzoefu wake unawakilisha hali ya wachezaji wengi wa Sudan waliolazimika kuikimbia nchi kutokana na vita vilivyoanza Aprili mwaka 2023, baada ya mvutano wa madaraka kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces kulipuka na kuwa mapigano ya wazi. Vita hivyo vimesababisha mauaji ya halaiki, ubakaji na vurugu za kikabila. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 40,000 wameuawa, huku zaidi ya milioni 14 wakilazimika kuyahama makazi yao, ingawa mashirika ya misaada yanasema idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi.
Licha ya hali hiyo ngumu, timu ya taifa ya Sudan, maarufu Falcons of Jediane, imeendelea kusimama imara. Timu hiyo chini ya kocha James Kwesi Appiah(mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana) ilifanikiwa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika licha ya kufanya mazoezi na kucheza mechi zote za kufuzu nje ya nchi. Sudan iliifunga Ghana bao 2-0, taifa kubwa la soka barani Afrika, na kuinyima nafasi ya kushiriki mashindano hayo.
Kwa Wasudan wengi, timu ya taifa ya soka imekuwa chanzo cha matumaini, umoja na faraja wakati wa vita. Kabla ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Algeria mjini Rabat, Morocco, mashabiki walionekana wakishangilia, wakipeperusha bendera za Sudan, kupiga honi na kupiga kelele za “Sudan!” huku wakielekea viwanjani.
Mchezaji wa timu ya taifa ya Sudan, Mohamed Abuaagla amesema kucheza na kushinda mechi kunaleta furaha kwa wananchi waliobaki nyumbani, akisema timu inajaribu kupanda “mbegu ndogo ya tabasamu” kwa watu wanaoteseka. Abuaagla pia alifichua kuwa alipoteza mjomba wake wakati wa vita, akisema walishindwa kumpeleka hospitalini kutokana na uharibifu uliosababishwa na mapigano.
Kutokana na kusimamishwa kwa ligi ya ndani, wachezaji wengi wa Sudan wamelazimika kucheza soka nje ya nchi, hasa Libya. Klabu kubwa za Sudan, Al Merrikh na Al Hilal, kwa sasa zinashiriki ligi ya Rwanda, baada ya awali kucheza nchini Mauritania ambako Al Hilal iliwahi kuwa bingwa.
Wachambuzi wanasema timu ya taifa ya Sudan imekuwa ishara isiyoegemea upande wa kisiasa, inayowaunganisha wananchi na kuwapa kitu cha kusherehekea, ingawa wanatahadharisha kuwa soka pekee haliwezi kumaliza vita hivyo vinavyohusisha wadau wengi wa ndani na kimataifa.
Katika mashindano ya AFCON 2025 yanayoendelea, Sudan ilipoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Algeria lakini ilirejea kwa ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Equatorial Guinea, licha ya kukumbwa na majeraha ya wachezaji kadhaa muhimu. Ushindi huo umeongeza matumaini ya kusonga mbele katika Kundi E, huku pambano muhimu dhidi ya Burkina Faso likitarajiwa.
Wachezaji wa Sudan wanasema huwa wanaingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kuwakilisha mateso na matumaini ya wananchi wao. Ammar Taifour amesema kabla ya kila mechi huwa anawaombea watu wa Sudan, akisisitiza kuwa wanastahili furaha na kwamba anafanya kila awezalo kuwaletea matumaini hayo kupitia soka.

.png)
Post a Comment