MTANGAZAJI

DEEPFAKE YATUMIWA KUWAUMIZA WANAFUNZI KISAIKOLOJIA


Baadhi ya shule katika maeneo mbalimbali nchini Marekani zinakabiliwa na changamoto mpya na hatari, baada ya wanafunzi kuanza kutumia teknolojia ya Akili Unde(AI), kubadilisha picha za kawaida za wenzao na kuzifanya kuwa picha au video bandia za kingono, maarufu deepfakes.

Taarifa zinaonesha kuwa kusambaa kwa picha hizi zilizochakachuliwa kunawaacha waathiriwa wakiwa na maumivu makubwa ya kisaikolojia, ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo, hofu na aibu. Katika tukio lililotikisa jamii ya huko Louisiana, picha zisizofaa zilizotengenezwa kwa AI zilisambaa katika shule ya sekondari hali iliyosababisha wavulana wawili kushtakiwa chini ya sheria mpya ya jimbo hilo. Ambapo wa waathiriwa alifukuzwa shule baada ya kuhusika katika ugomvi unaohusishwa na tukio hilo.

Maafisa wa usalama wanasema ingawa kubadilisha picha si jambo jipya, kuibuka kwa AI kumerahisisha zaidi uhalifu huu. Afisa wa polisi wa Lafourche, Craig Webre, amesema mtu yeyote sasa anaweza kuunda picha hizo bila ujuzi wowote wa kitaalamu, na akawataka wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu hatari hizo.

Majimbo kadhaa nchini Marekani yameanza kupitisha sheria kali dhidi ya deepfakes. Kufikia mwaka 2025, takribani nusu ya majimbo yalikuwa yameweka sheria zinazolenga matumizi mabaya ya AI, hasa pale inapohusisha kuiga unyanyasaji wa kingono kwa watoto. Tayari kesi kama hizi zimeripotiwa pia katika majimbo ya Florida, Pennsylvania, California na Texas.

Wataalamu wa masuala ya unyanyasaji mtandaoni wanaonya kuwa shule nyingi bado hazijajiandaa vya kutosha kukabiliana na tatizo hili. Sameer Hinduja, mtaalamu wa utafiti wa unyanyasaji wa kidijitali, anasema wanafunzi wakiona walimu na shule hawana ufahamu, hujiona wako huru kufanya vitendo hivyo bila kuadhibiwa.

Takwimu kutoka kituo cha kitaifa cha watoto waliopotea na kunyanyaswa zinaonesha ukubwa wa tatizo hili, baada ya idadi ya picha za unyanyasaji wa watoto zinazotengenezwa kwa AI kuongezeka kutoka 4,700  mwaka 2023 hadi zaidi ya 440,000 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2025.

Wataalamu pia wanasema madhara ya deepfakes ni makubwa kuliko unyanyasaji wa kawaida, kwa kuwa picha na video hizo huendelea kusambaa na kujitokeza tena mara kwa mara, na hivyo kuongeza maumivu kwa waathiriwa.

Wazazi wanahimizwa kuanza mazungumzo ya wazi na watoto wao kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na hatari za deepfakes. Wataalamu wanashauri watoto waelezwe kuwa wanaweza kuripoti au kuzungumza na wazazi wao bila kuogopa kuadhibiwa.

Kwa sasa, wadau wa elimu, wazazi na vyombo vya sheria nchini Marekani wanakubaliana kuwa mapambano dhidi ya deepfakes shuleni yanahitaji ushirikiano wa pamoja, elimu kwa wanafunzi, na utekelezaji madhubuti wa sheria.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.