Uamuzi wa kuivunjwa iliyokuwa Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania uliotangazwa hivi karibuni na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini Tanzania (RITA) umepokelewa kwa hisia tofauti na miongoni mwa waumini wa kanisa hilo nchini humo na nje ya Tanzania.Kumekuwepo na mijadala mbalimbali tangu kutolewa kwa agizo hilo na Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi na kisha kuonekana kwenye vyombo vya habari Tanzania na kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Youtube ya RITA, Feb 24 mwaka huu, kufuatia
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) kubaini
Bodi hiyo kushindwa kusimamia ipasavyo mali na majukumu yake na hivyo
kutoa siku saba kwa uongozi wa mpya wa kanisa hilo kuwasilisha majina kumi (10) ya waumini watakaopendekezwa kuwa wajumbe wapya wa kamati ya mpito
itakayosimamia mali za kanisa hilo hadi itakapopatikana Bodi mpya ya
Wadhamini.
Bw.
Kanyusi alieleza kuwa ripoti aliyoipokea ni ya ukaguzi maalum wa kiuchunguzi wa mali
za Kanisa la Waadiventista wa Sabato Tanzania uliofanywa na Ofisi ya CAG kufuatia malalamiko
yalivyowasilishwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo katika ofisi ya
kabidhi Wasii Mkuu na Msajili wa Jumuiya za Kiraia Wizara ya Mambo ya
ndani ya nchi wakilalamika kuwepo kwa ubadhirifu wa mali za kanisa na
matumizi mabaya ya madaraka.
Baada ya agizo hilo baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakiendelea na mijadala kwenye mitandao ya kijamii wakihoji na kutaka kufahamu undani kuhusu tuhuma hizo, nani wanaohusishwa na tuhuma hizo katika miongoni mwa wajumbe ingawa baadhi yao hata hawafahamu muundo,
majina ya wajumbe wa bodi ya wadhamini ya kanisa hilo nchini Tanzania na jinsi inavyotekeleza majukumu yake.
Kanyusi amebainisha kuwa, taarifa hiyo ni hatua muhimu iliyochukuliwa kwa kushirikiana na Msajili wa Jumuiya za Kiraia Emmanuel Kihampa kutoka wizara ya mambo ya ndani kuamua kufanyika kwa ukaguzi maalum wa kiuchunguzi ili kujiridhisha na usahihi na ukweli wa malalamiko yaliyowasilishwa na waumini wa kanisa hilo huku akifafanua kuwa, taarifa hiyo itafanyiwa kazi kwa haraka na kuwasilishwa kwa vyombo vingine vya kiuchunguzi ili wale wote waliobainika katika taarifa ya CAG kuhusika na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka na mali za taasisi hiyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa barua ya Msajili wa Jumuia za Kiraia ya Februari 21,2025 yenye Kumb. Na. SA. 5333/I/44 iliyosainiwa na Emmanuel Kihampa, ikieleza mambo kadhaa ikiwemo kufanyika kwa kikao kati ya uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Tanzania na baadhi ya waumini wa kanisa hilo Agosti 17, 2021 baada ya kupokea malalamiko na tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa na waumini hao, ikiwemo ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na matumizi mbaya ya fedha na maliza kanisa hilo hususani Unioni ya Kusini mwa Tanzania ( STUM)
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini iliyovunjwa walikuwa ni viongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Tanzania katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 ambao miongoni mwao wameshastaafu ama kupewa majukumu mengine baada ya kuchaguliwa viongozi wapya kwa utaratibu wa kanisa hilo ulimwenguni hata kabla ya kuvunjwa kwa bodi hiyo.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi na kisha kuvunja Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini humo toka kanisa hilo lilipoanzisha utume wake mwaka 1903 baada ya Wamishenari kutoka Ujerumani kufika Tanzania Novemba 1903.
Kwa mujibu wa takwimu za Kanisa hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani za mwaka 2024 zinaonesha kuwa kuna idadi ya waumini 880,455 wa Unioni Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania (NTUC) na 266,272 katika Unioni ya Kusini mwa Tanzania ( STUM)
Post a Comment