MTANGAZAJI

ZAIDI YA SIMU BILIONI MOJA ZA ANDROID ZIKO HATARINI


 

Zaidi ya asilimia 40 ya vifaa vya Android duniani kote havipokei tena masasisho muhimu ya usalama, hali inayowaacha zaidi ya watumiaji bilioni moja katika hatari ya kushambuliwa na programu hasidi na ujasusi, kwa mujibu wa kampuni ya Google.

Tatizo hili si hitilafu ya ghafla, bali ni hali iliyoendelea kwa muda. Takwimu za usambazaji wa Android zinaonyesha kuwa watumiaji wengi bado wanatumia matoleo ya zamani ambayo Google haiungi mkono kikamilifu tena. Google imesisitiza kuwa mkanganyiko wa hivi karibuni kuhusu tarehe za masasisho ya mfumo wa Google Play ulikuwa wa muonekano tu na haukuathiri usalama wa vifaa.

Hata hivyo, tatizo kuu ni kwamba simu zinazotumia Android toleo la 12 au matoleo ya zamani sasa ziko nje ya wigo wa ulinzi kamili wa usalama.

Kwa mujibu wa ripoti ya Forbes,iliyochapishwa Februari 5, mwka huu ni takribani asilimia 58 pekee ya vifaa vinavyotumia Android toleo la 13 au toleo jipya zaidi. Kufikia Desemba mwaka 2025, Android 16 ilikuwa imewekwa kwenye asilimia 7.5 tu ya simu. Android 15 ilikuwa na asilimia 19.3 ya vifaa, Android 14 asilimia 17.9, na Android 13 asilimia 13.9. Matoleo hayo manne ni muhimu kwa sababu Google haitoi tena masasisho muhimu ya usalama wa kiwango cha mfumo kwa Android 12 au matoleo ya zamani.

Hali hiyo ina maana kuwa zaidi ya asilimia 40 ya simu za Android zinazotumika sasa hazina ulinzi kamili wa mfumo wa uendeshaji, na hazina njia ya wazi ya kupokea marekebisho ya mashambulizi mapya yanayogunduliwa. Google imesema kuwa vifaa vya zamani bado vinapata ulinzi wa kiwango fulani kupitia Google Play Protect, ambayo inaendelea kusaidia vifaa tangu Android 7 kwa kutoa masasisho ya alama za programu hasidi na uchunguzi wa wakati halisi.

Pengo la usalama linaongezeka kutokana na baadhi ya wazalishaji kupunguza muda wa usaidizi wa vifaa vyao. Samsung imethibitisha kuwa Galaxy S21, S21 Plus na S21 Ultra hazipokei tena masasisho ya Android au ya usalama. Aidha, mfululizo wa Galaxy S22 pamoja na Galaxy S21 FE sasa utapokea masasisho ya kila robo mwaka badala ya kila mwezi, hatua inayoongeza muda wa hatari dhidi ya udhaifu mpya wa kiusalama.

Kwa mujibu wa Gulf News, tofauti na Apple ambayo inadhibiti moja kwa moja masasisho ya vifaa na programu zake, mfumo wa Android hutegemea wazalishaji binafsi kusambaza viraka vya usalama. Mara nyingi simu huachwa baada ya miaka michache, jambo linalowaacha watumiaji katika hatari ya mashambulizi ya mtandao.

Kuhusu mkanganyiko wa tarehe za Google Play, Google imeeleza kuwa baadhi ya watumiaji waliona tarehe ya sasisho ikirudi nyuma kutoka Januari 2026 hadi Novemba 2025. Kampuni hiyo imesisitiza kuwa hilo lilikuwa tatizo la muonekano tu na halikuathiri utendaji wala usalama wa kifaa, na kwamba inafanyia kazi marekebisho ya kuonyesha tarehe sahihi.

Kwa sasa, simu zisizoweza kuendesha Android 13 au toleo jipya zaidi hazipokei tena masasisho muhimu ya usalama wa mfumo, hali inayowaacha watumiaji na chaguo chache zaidi ya kubadilisha vifaa visivyoungwa mkono. Wachambuzi wanasema hata simu mpya za kiwango cha kati zilizo na usaidizi wa programu unaoendelea zinaweza kutoa ulinzi bora zaidi kuliko simu za zamani za kiwango cha juu zilizopitwa na wakati.





No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.