DHORUBA YA THERUJI NA UPEPO YAWAKABILI WAMAREKANI
Dhoruba kali ya majira ya baridi imetishia kusababisha hali hatarishi ya theluji yenye upepo mkali, usafiri mgumu na kukatika kwa umeme katika maeneo ya magharibi kati mwa Marekani, huku sehemu nyingine za nchi hiyo zikijiandaa kukabiliana na kushuka kwa kasi kwa joto, upepo mkali na mchanganyiko wa theluji, barafu na mvua.
Kwa mujibu wa Huduma ya Taifa ya Hali ya Hewa ya Marekani, theluji nzito na upepo mkali vilianza kuenea Jumapili katika maeneo ya kaskazini , na kusababisha onyo la hali ya kutoona kabisa barabarani, hali inayoweza kufanya safari kuwa hatari au hata kutowezekana. Baadhi ya maeneo karibu na Maziwa Makuu yanatarajiwa kupata zaidi ya futi moja ya theluji,huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka maradufu.
Takriban wateja 350,000 walikosa umeme asubuhi ya Jumatatu, wengi wao wakiwa katika jimbo la Michigan. Aidha, safari zaidi ya 1,600 za ndege zilicheleweshwa na zaidi ya 450 zikiahirishwa katika viwanja vya ndege kote Marekani kutokana na hali mbaya ya hewa.
Hali ya theluji yenye upepo mkali iliendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Iowa, hasa vijijini, huku theluji ikivuma kwa nguvu. Huduma ya hali ya hewa pia imetoa onyo la theluji ya kati futi 1 hadi 3 pamoja na upepo mkali unaofikia maili 75 kwa saa magharibi mwa New York, na hali kama hiyo ikitarajiwa huko Michigan na Ohio karibu na Ziwa Erie.
Gavana wa New York, Kathy Hochul, amewaonya wakazi wa eneo la Buffalo kuepuka safari zisizo za lazima kutokana na hatari ya hali ya kutoona kabisa barabarani.
Mpaka mkali wa hewa baridi umesababisha kushuka kwa ghafla kwa joto katika maeneo ya kati ya Marekani, ambapo baadhi ya sehemu zimepungua hadi nyuzi 50 za Fahrenheit ikilinganishwa na siku iliyotangulia. Huduma ya hali ya hewa imeonya kuhusu baridi kali inayochangiwa na upepo, inayoweza kufikia hadi nyuzi hasi 30 za Fahrenheit katika North Dakota na Minnesota.
Kusini mwa nchi, wataalamu wa hali ya hewa wanasema dhoruba kali za radi zinaashiria kuwasili kwa hewa baridi kali itakayomaliza siku kadhaa za joto kali. Majimbo ya Georgia, Texas na Arkansas yanatarajiwa kushuhudia kushuka kwa haraka kwa joto kuanzia Jumatatu hadi Jumanne.
Mamlaka za hali ya hewa zinasema dhoruba hii inatarajiwa kuimarika zaidi inaposogea mashariki, ikichochewa na mgongano wa hewa kali ya baridi kutoka Kanada na hewa ya joto iliyodumu Kusini mwa Marekani, huku wananchi wakishauriwa kufuatilia tahadhari rasmi na kuchukua tahadhari zinazohitajika

.png)
Post a Comment