WACHUNGAJI 19 WAADVENTISTA WAONDOLEWA KAZINI
Konferensi ya Central Rift Valley ya Kanisa la Waadventista wa Sabato iliyoko Nakuru, Kenya (CRVC) imewafuta kazi wachungaji 19 kwa madai ya utovu wa nidhamu, kukiuka taratibu na miongozo ya kanisa hilo ikiwemo kuunda taasisi nyingine ya kiutawala.
Uamuzi huo umetolewa baada ya CRVC kuwatuhumu wachungaji hao kwa kukiuka mwongozo na mafundisho ya kanisa huku wakijiunga na taasisi nyingine kinyume na utaratibu.
Taarifa zinazoelezwa katika waraka kutoka CRVC zinaonesha kuwa wachungaji hao walijipanga chini ya mwavuli unaoitwa Mid Rift Valley Union of Churches Conference, taasisi ambayo haitambuliwi na mwajiri wao kuwa sehemu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato.
“Barua hii ni taarifa rasmi kutoka kwa Konferensi ya Central Rift Valley (CRVC) chini ya kumbukumbu ya kikao cha Excom namba 26Excom 010 cha Februari 1, 2026, kuarifu makanisa yote yaliyo chini ya mamlaka yake kwamba wachungaji hao 19 wamefutwa kazi na hati zao za utumishi pamoja na leseni zao zimeondolewa mara moja,” inasema sehemu ya waraka huo wa Februari 3, 2026.
Hata hivyo, mmoja wa wachungaji waliotajwa kwenye barua ya kufukuzwa, Mchungaji Daniel Kerochi, katika mahojiano ya simu na gazeti la The Star, alikanusha madai kwamba yeye na wengine 18 wameunda kundi la uasi au kufanya kitendo chochote cha kupotoka kiimani.
“Hatukuunda kundi lolote la uasi; hilo si kweli. Kwa hakika, bado tunafuata sera za Kanisa la SDA kikamilifu,” alisema Mchungaji Kerochi.
Kerochi aliongeza kuwa wachungaji waliotajwa kwenye barua hiyo bado wanatambua mamlaka ya Makao Makuu ya Kanisa la Waadventista Ulimwenguni (GC) yaliyoko Silver Springs, Maryland, Marekani, na kwamba hawawajibiki kwa barua ya kufukuzwa kutoka CRVC.“Ni tabia yao kuwafukuza watu; hatuwezi kujadiliana nao. Wachungaji wetu ni safi,” alisema Kerochi.
Kwa mujibu wa waraka huo, watu waliotajwa hawatambuliki tena kama wachungaji, wafanyakazi, au wawakilishi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato chini ya CRVC.
“Hivyo basi, makanisa yote yanaelekezwa kwamba watu hawa hawana mamlaka ya kushiriki katika shughuli zozote za kiroho, kiutawala, au za kichungaji ndani ya Kanisa lolote la Waadventista wa Sabato chini ya CRVC kutokana na utovu wao mkubwa wa nidhamu na kuunda shirika la uasi kinyume na Sera na Mwongozo wa Kanisa,” waraka unasema.
Hatua hii inafanana na mgawanyiko uliotokea miaka michache iliyopita ambapo Konferensi ya Kati ya Kenya (CKC) iliyoko Nairobi ilipitia migogoro ya ndani iliyosababisha kuundwa kwa Konferensi ya Nairobi Cosmopolitan (NCC) ambayo sasa inaongoza makanisa kadhaa.
Waraka huo, uliotiwa saini na Kaimu Katibu Mkuu wa CRVC, Olgar Kemuma, unasema kuwa kufutwa kwa mikataba ya wachungaji hao kunajumuisha, lakini hakujifungi tu kwenye kuhubiri, kufundisha, kuendesha ibada na, kuongoza programu, kukusanya zaka na sadaka, kufungua akaunti za benki, au kuwakilisha Kanisa hilo kwa namna yoyote ile.
Makanisa na waumini wanaelekezwa kutowaruhusu watu hao kufanya au kushiriki katika shughuli zozote ndani ya makanisa yetu. “Ushirikiano wenu katika jambo hili ni muhimu ili kudumisha utaratibu, umoja, na utii kwa sera za kanisa.”
Ikumbuke kuwa Juni 2025, CRVC iliwasimamisha kwa muda wachungaji 25 kutokana na kutokufuata sera na taratibu muhimu za kanisa la Waadventista wa Sabato ikiwemo kushindwa kufuata Sera ya Utendaji ya Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD), Biblia, Mwongozo wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, pamoja na Kanuni za CRVC.
Katika barua ya Juni 29, 2025 iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wa CRVC,wakati huo Mchungaji Philip Isika, Kamati Kuu ya Utendaji iliazimia kuwasimamisha wachungaji hao kwa kipindi cha mwezi mmoja kusubiri uchunguzi zaidi. Uamuzi huo ulipitishwa chini ya kumbukumbu ya kikao namba 25 Excom 032 wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya CRVC.

.png)
Post a Comment