IMAMU WA ZAMANI JELA MIAKA 80 KWA UNYANYASAJI WA KIONGONO KWA WATOTO
Imamu wa zamani wa Texas, Marekani na mwalimu wa Qurani mtandaoni, Wisam Sharieff, amehukumiwa kifungo cha miaka 80 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa yanayohusiana na unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama ya shirikisho, Sharieff alihukumiwa Jumatano ya Januari 28 mwaka huu, katika Mahakama ya Wilaya ya Kaskazini ya Alabama, zaidi ya miezi sita baada ya kukiri mashtaka matatu ya shirikisho ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto. Aidha, ameamriwa kulipa dola za Kimarekani 135,000 kwa mfuko wa kusaidia waathirika wa unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Mahakama ilielezwa kuwa Sharieff alipanga njama pamoja na Blake Miller Barakat, mwanamke wa jimbo la Alabama anayelezwa kuwa mpenzi wake aliyekuwa akimfundisha, kumlazimisha mtoto wa Barakat kushiriki katika vitendo vya kingono kwa lengo la kutengeneza ponografia. Mshirika wake huyo, Barakat, alihukumiwa kifungo cha miaka 70 mwezi Oktoba mwaka jana.
Uchunguzi wa FBI ulibaini kuwepo kwa mawasiliano ya faragha kupitia mtandao wa Telegram, ambapo Sharieff alidaiwa kutuma video chafu zake mwenyewe, huku mama huyo akituma video za mtoto wake akitazama ponografia ya watu wazima. Vifaa vya kielektroniki na vifaa vya kingono pia vilikamatwa nyumbani kwa Barakat.
Kukamatwa kwa Sharieff miaka miwili iliyopita kulizua hasira na maswali makubwa ndani ya jamii ya Waislamu nchini Marekani, hususani kuhusu uwajibikaji wa viongozi wa kiroho wanaotuhumiwa kutumia vibaya mamlaka yao. Kabla ya kukamatwa, Sharieff alikuwa mwalimu maarufu wa Qurani katika taasisi ya AlMaghrib, na alijulikana kwa kuanzisha programu ya Quran Revolution. Taasisi hiyo ilisitisha ajira yake mara baada ya kuchunguza tuhuma hizo.
Akiwa gerezani, Sharieff aliandika kitabu cha watoto na makala za binafsi, na katika chapisho la blogu mwaka 2025 alidai tabia yake ilisababishwa na uraibu wa ponografia. Hata hivyo, wataalamu wa afya ya akili na kingono wameonya kuwa matumizi ya neno “uraibu” hayapaswi kutumika kupunguza uwajibikaji, hasa pale inapohusisha unyanyasaji kwa watoto.
Wataalamu nchini Marekani wanasema jamii za kidini, zikiwemo za Kiislamu, bado zinakabiliwa na changamoto ya kujenga mifumo madhubuti ya uwajibikaji ili kuzuia na kushughulikia vitendo vya unyanyasaji wa kingono na kiroho.

.png)
Post a Comment