WAADVENTISTA WAPINGA PENDEKEZO LA MAPUMZIKO YA JUMAPILI
Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Divisheni ya Amerika ya Kaskazini (NAD) limetoa msimamo kuhusu pendekezo la mapumziko ya jumapili kwa kuwa linainua wasiwasi mkubwa kuhusu uhuru wa kidini nchini Marekani.
Kupitia tovuti yake na mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram NAD imeeleza kuwa hati ya pendekezo la mapumziko ya jumapili iliyotolewa hivi karibuni na The Heritage Foundation ya nchini Marekani la mapumziko ya Jumapili linazua wasiwasi mkubwa kuhusu uhuru wa kidini.
"Pendekezo lililotolewa na shirika moja la utetezi lililoko Washington, D.C., la kutambua kisheria na kutekeleza ‘siku ya mapumziko ya pamoja’ linaonyesha kupuuzwa kwa kutisha kwa uhuru wa kidini wa Wamarekani wote" imeleza taarifa hiyo.
Hati ya The Heritage Foundation iitwayo ‘Saving America by Saving the Family’ yenye kurasa 168 inazitaka serikali za majimbo na manispaa nchini Marekani kuweka vikwazo kwa shughuli za biashara siku ya Jumapili kama njia ya kuhamasisha ushiriki wa kiroho na kutoa siku ya kawaida ya kupumzika kwa wafanyakazi wa Marekani.
Januari 8, mwaka huu The Heritage Foundation iliwasilisha hati hiyo kwa kwa watunga sera wa Marekani, ikiwemo Congress na utawala wa Rais Trump, kama mwongozo wa sera za familia na mapumziko ya Jumapili.
“Waadventista wa Sabato wanaamini kwamba watu wote wameumbwa kwa mfano wa Mungu na wamepewa uhuru wa kuabudu kulingana na dhamiri zao. Kwa zaidi ya miaka 160, Kanisa limekuwa likipinga kwa nguvu aina yoyote ya sheria ya Jumapili. Waadventista daima wameelewa sheria hizi iwe katika ngazi ya mtaa, jimbo, au serikali kuu kama juhudi za kulazimisha dhamiri, hata pale zinapotetewa kwa sababu za nje kama vile kulinda afya ya jamii na familia.”
Tamko hilo limeendelea kueleza kuwa pendekezo hili jipya la ‘siku ya mapumziko ya pamoja’ halipatani kabisa na urithi mpana wa Marekani wa kulinda uhuru wa kidini kwa raia wake wote, bila kujali imani au kutokuwa na imani. Linawakilisha shauku hatari ya kutumia nguvu za serikali kusukuma malengo ya kidini. Kuweka vikwazo kwa shughuli za kibiashara siku ya Jumapili pia kunaleta changamoto kubwa za kiutendaji kwa waumini wa dini ambazo hawaabudu Jumapili, wakiwemo Waadventista wa Sabato na Wayahudi wa Orthodox.
“Sheria za Jumapili zinapingana na marekebisho ya kwanza ya Katiba ya Marekani, ambayo yanahifadhi uhuru wa kidini kwa Wamarekani wote kwa kuitaka serikali ibaki bila upendeleo kati ya dini mbalimbali. Viongozi wetu wa kanisa katika Divisheni ya Amerika Kaskazini na konferensi wataendelea kutetea bendera ya ukweli na uhuru wa kidini, wakipinga vikali pendekezo hili na hatua nyingine zozote zinazofanana nalo.” Imemaliza taarifa hiyo.

Post a Comment