MTANGAZAJI

KANISA LA WAADVENTISTA LACHUNGUZA UTAPELI WA CRYPTO

 

 
Kanisa la Waadventista wa Sabato limetangaza uchunguzi wa wazi kuhusu shughuli za biashara ya fedha za kidijitali (crypto-trading) ambapo baadhi ya waumini nchini Kenya walipoteza mamilioni ya fedha baada ya jukwaa la mtandaoni kuporomoka.
 
Kuporomoka kwa jukwaa la biashara ya sarafu za kidijitali na forex lililokuwa likitangazwa na kiongozi mmoja mwandamizi wa kanisa kuliwaacha baadhi ya Wakenya wakiripoti hasara za kifedha zinazokadiriwa kufikia mamilioni ya shilingi.
 
Jukwaa hilo lilifungwa ghafla baada ya watumiaji kugundua kuwa tovuti yake ilitoweka na walielekezwa kwenye jukwaa jipya lililohitaji ada ya usajili ya angalau shilingi za Kenya 24,000. Mchungaji Paul Mwangi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Konferensi ya Kati ya Kenya (CKC) wakati huo, ambayo inasimamia makanisa ya Nairobi, Kiambu, Machakos na kaunti jirani, ni miongoni mwa waliokiri kupoteza mamilioni katika ulaghai huo, hata baada ya kuwahamasisha waumini wengi kujiunga na biashara hiyo.
 
Mchungaji Mwangi alikuwa Katibu mtendaji wa Unioni Konferensi ya  Unioni Konferensi ya Kenya Mashariki ya Kanisa la Waadventista East (EKUC), eneo lingine la kiutawala linachosimamia karibu nusu ya makanisa ya Waadventista nchini Kenya, na tangu wakati huo amejiuzulu kwa muda kupisha uchunguzi unaoendelea.
 
Katika video ya Disemba 14, 2025, Kiongozi huyo wa dini alisema alitambulishwa kwenye Optcoin na watu wengine waliomhimiza kuhamisha uwekezaji kutoka majukwaa mengine ya crypto na forex kwenda kwenye jukwaa hilo. Baadaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kanda ya Kenya, nafasi iliyomfanya kuwa mwakilishi mkuu na kusababisha wengine wengi kujiunga. Mwangi alieleza kupoteza zaidi ya dola 735,000 za  Marekani, sawa na takribani shilingi milioni  94 za Kenya, na kushindwa kutoa fedha zake.
 
Katika tangazo kwa umma la Februari 26 , 2026, Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD), chombo kinachosimamia shughuli za kiutawala za kanisa katika eneo hilo, kilitoa ratiba ya uchunguzi huo wa wazi.
 
ECD pia itatumia tume hiyo kusikiliza na kuamua rufaa ya wachungaji 19 waliotimuliwa kazi na Konferensi ya Central Rift Valley ya Nakuru hivi karibuni  kwa madai ya utovu wa nidhamu, kukiuka taratibu na miongozo ya kanisa hilo ikiwemo kuunda taasisi nyingine ya kiutalawa.
 
ECD ni sehemu ya kiutawala ya Makao Makuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani (GC) yenye makao yake makuu Maryland, Marekani na kitengo cha juu cha utawala wa kanisa hilo. Makao Makuu ya ECD yako Rongai na inasimamia nchi 11 katika kanda hiyo.
 
“ Tume ya ECD kuhusu masuala ya Opticoin/Wealth Sharing na Konferensi ya Central Rift Valley inapenda kushiriki miongozo yake ya uendeshaji,” sehemu ya tangazo hilo ilieleza.
 
Vikao  vya Tume itafanyika yalipo makao makuu ya ECD , Advent Hill, Ongata Rongai, ambapo Machi 2, 2026 ilikuwa  siku ya utangulizi na kikao cha awali cha maafisa wa ECD na Tume. Machi 3, 2026, timu itapokea mawasilisho yanayohusiana na suala la Opticoin/Wealth Sharing kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana na kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 11:30 jioni.
 
Jumatano, Machi 4, 2026, Tume itapokea mawasilisho yanayohusiana na suala la wachungaji 19 kwa muda huo huo. Siku inayofuata, Alhamisi, Tume itafanya majadiliano, na Ijumaa itakutana kuandaa mapendekezo.
 
Katibu wa Tume, Tom Ogal, alisema kuwa mawasilisho yote lazima yawe kwa maandishi, yatiwe saini pamoja na jina na namba ya simu ya mtoa taarifa, na yaambatane na ushahidi wa maandishi pale inapowezekana. Wanaotaka kutuma mawasilisho kwa barua pepe wanaweza kutumia ogalt@ecd.adventist.org.
 
Ogal aliongeza kuwa wale wanaotaka kuwasilisha taarifa bila kufika mbele ya Tume wanaweza kufanya hivyo mradi mawasilisho yao yawe kwa maandishi, yamesainiwa na kuambatanishwa na ushahidi husika. Wale watakaofika mbele ya Tume watawasilisha hoja zao za mdomo kwa kuzingatia nyaraka walizowasilisha kwa maandishi. Makundi yaliyoathirika yanaweza kuteua wawakilishi wachache kuwasilisha hoja kwa niaba yao.
 
Aidha, Ogal alisema Tume inaweza kuwaalika watu au makundi maalum yenye maslahi kujitokeza mbele yake pale itakapohitajika.
 
Novemba 6, 2025, muda mfupi kabla ya jukwaa hilo kuporomoka, ECD ilitoa barua ya tahadhari kwa viongozi waandamizi ikionya dhidi ya kuhusika katika shughuli za kifedha zisizo za maadili au zisizo halali.
 
“ Hakuna mhudumu au mfanyakazi wa kanisa atakayeshiriki, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, katika kuendeleza au kuwezesha shughuli yoyote ya uwekezaji isiyo ya kimaadili, isiyo na leseni au ya ulaghai, iwe ana kwa ana, kupitia mashirika, au kupitia majukwaa ya mtandaoni,” barua hiyo ilieleza.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.