WANAUME WATAKIWA KUVUNJA UKIMYA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wanaume kutoa taarifa kwenye mamlaka husika kuhusu ukatili wanaofanyiwa ili kutokomeza matukio ya ukatili nchini.
Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipotoa tamko kuhusu Vitendo vya Ukatili katika jamii mbele ya waandishi wa habari.
Gwajima amesema vitendo vya ukatili vimezidi kuongezeka nchini Tanzania akitolea mifano mbalimbali iliyotokea hivi karibuni ya wanafamilia kufanyiana vitendo vya kikatili.
Amesema ukatili haufanywi kwa wanawake na watoto tu lakini hata kwa makundi mengine ikiwemo wanaume lakini wengi wao wamekuwa wakikaa kimya.
"Wanaume msione aibu, muache kukaa kimya dhidi ya vitendo vya ukatili mnavyofanyiwa. Toeni taarifa mapema kwa mamlaka husika muweze kupata msaada ili kuzuia madhara zaidi kutokea" amesema Gwajima.
Amezitaja sababu za ukatili huu ni pamoja na migogoro ya kifamilia ikiwemo kugombea mali, matatizo ya kisaikolojia na jamii kutotekeleza wajibu wake wa kutunza na kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi ya familia.
Dkt Gwajima amesema Wizara itaendelea kuchukua jitihada zote kuhakikisha ukatili unatokomezwa kwa makundi yote, lakini jamii pia ina jukumu la kuwalinda makundi yote.
Post a Comment