MTANGAZAJI

SERIKALI YA TANZANIA YATANGAZA VITA NA WAHALIFU MTANDAONI


 Serikali ya Tanzania imeanza mkakati wa kushughulika na watu wanaotoa lugha za matusi, kashfa na utapeli mitandaoni ambapo mpaka sasa genge la watu 17 wanaoongoza genge la uhalifu mitandaoni waliokuwa wamejificha mkoani Morogoro wameshakamatwa na muda wowote watapandishwa mahakamani.

Taarifa hiyo imetolewa na  Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini humo  Dkt. Faustine Ndugulile (pichani) katika hafla ya makabidhiano ya mikataba ya  miradi minne ya miundombinu ya mawasiliano yenye thamani ya shilingi bilioni 7.5 baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na wakandarasi ambao  ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Raddy Fibre Solution Ltd katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.


Ameongeza kuwa Serikali ina nia njema ya kujenga mazingira wezeshi ya kuweza kutumia mitandao ya mawasiliano na katiba ya nchi inaruhusu wananchi kukosoa kwa lugha ya staha,huku akisisitiza kuwa lugha za matusi, kashfa na kejeli hazitovumilika.

 Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wasipokee maelekezo yeyote kuhusu miamala binafsi kwa njia ya simu bali njia sahihi ni kwenda kwenye vituo vya mawakala vinavyotambulika na vilivyosajiliwa na makampuni ya simu.


“Tunataka kuimarisha mifumo ya mawakala wa makampuni ya simu ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua mawakala ambao sio waaminifu”, Dkt. Ndugulile.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.