VIPINDI VYA MICHEZO SHULENI NCHINI TANZANIA SASA NI LAZIMA
Serikali ya Tanzania kupitia kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega ameagiza viongozi na wasimamizi wa shule zote nchini humo kusimamia vyema vipindi vya michezo shuleni.
Ametoa agizo hilo alipokua katika shule ya Sekondari Dodoma ambapo Naibu Waziri Ulega ameipongeza shule hiyo kwa kuwa na ratiba ya vipindi vya michezo ambayo inatekelezwa na amesisitiza ratiba hiyo iendelee kuzingatiwa.
"Vipindi vya michezo shuleni viheshimiwe, wanafunzi wapate nafasi ya kucheza ili waimarishe afya zao, pia wakuze na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika maisha yao baada ya shule pamoja na kulitumikia Taifa katika Sekta ya michezo", alisema Mhe.Ulega.
Ulega ameongeza kuwa Mikoa na
Halmashauri zote lazima zitenge fedha kidogo katika bajeti zao kwa ajili ya
kuwezesha majukumu ya Maafisa Michezo na Utamaduni katika maeneo yao.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Maduka Kessy ameeleza kuwa michezo katika mkoa huo inaenda vizuri, huku akitolea mfano timu ya Dodoma Jiji inayoshiriki ligi kuu pamoja na Dodoma Queens inayoshiriki ligi ya wanawake.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuahidi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya michezo, tunaahidi tutaitumia vizuri katika kuendeleza michezo hapa mkoani na nchi kwa ujumla" alisema Dkt. Kessy.
Mkuu wa shule ya Sekondari Dodoma, Amani Mfaume amesema shule hiyo ni kituo cha michezo kwa mkoa wa Dodoma na imekuwa ikifanya vizuri katika michezo mbalimbali inayofanyika kila mwaka.
Post a Comment