MFUMO WA UDHIBITI KWA WATOTO WAMWOKOA BINTI
Siku iliyokusudiwa kuwa ya familia na mapumziko iligeuka kuwa ya hofu na wasiwasi huko Texas,Marekani baada ya msichana mwenye umri wa miaka 15 kutorejea nyumbani alipokuwa amemtoa mbwa wao matembezini, kwa mujibu wa maafisa wa usalama.
Ofisi ya Polisi wa Kaunti ya Montgomery imesema kuwa baada ya kupita muda wa kawaida wa matembezi hayo, wazazi wake walianza kuwa na wasiwasi. Baba wa msichana huyo alitumia mfumo wa udhibiti wa wazazi kwenye simu ya binti yake na kufuatilia mahali alipo, hadi eneo la faragha lililozungukwa na miti katika Kaunti ya Harris, takribani maili mbili kutoka nyumbani kwao mjini Porter,umbali wa maili 30 kutoka jiji la Houston.
Baba huyo alifuata alama ya eneo hilo kwenye simu yake hadi msituni, ambako alimkuta binti yake pamoja na mbwa wao ndani ya gari aina ya pickup, akiwa na mwanaume asiyejulikana ambaye alikuwa nusu uchi. Baba huyo alimsaidia binti yake kutoroka kutoka kwenye gari hilo na mara moja kuwasiliana na vyombo vya sheria.
Kwa msaada wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio, polisi waliweza kulipata gari hilo na kumtambua dereva wake kuwa ni Giovanni Rosales Espinoza, mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Porter. Familia ya msichana huyo imeviambia vyombo vya habari kuwa hawakuwa wakimfahamu mtuhumiwa huyo. Msichana na familia yake hawajatambuliwa hadharani hadi sasa.
Uchunguzi wa polisi umebaini kuwa mtuhumiwa alimtishia msichana huyo kwa kisu na kumteka nyara kutoka barabarani. Espinoza alikamatwa bila upinzani na kushtakiwa kwa makosa ya utekaji nyara wa hali ya juu pamoja na kufanya vitendo visivyo vya maadili kwa mtoto.
Afisa wa Polisi wa Kaunti ya Montgomery, Wesley Doolittle, amewapongeza maafisa na wachunguzi wa idara yake kwa kazi yao ya haraka iliyowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, na kuhakikishia jamii kuwa idara hiyo imejizatiti kulinda usalama wa familia.
Akizungumzia tukio hilo, Doolittle alisema, “Krismasi ni siku iliyokusudiwa kuwa ya furaha, lakini mtu huyu alichagua kuivunja furaha hiyo kwa kumlenga mtoto.”
Kwa sasa, Giovanni Rosales Espinoza anashikiliwa bila dhamana katika Gereza la Kaunti ya Montgomery, huku ikibainika kuwa haijulikani iwapo ana wakili anayemwakilisha kwa wakati huu.

.png)
Post a Comment