MTANGAZAJI

TAUS WAFANYA MAOMBI YA KUOMBEA TANZANIA

 


Umoja wa Watanzania Waadventista waishio nchini Marekani na Canada (TAUS) umeendesha maombi ya kwa ajili ya kuombea amani Tanzania baada ya sintofahamu ya huzuni iliyotanda  kutokana na mauaji ya watanzania  yaliyotokea baada ya maandamano ya vijana wa GenZ kupinga uchaguzi mkuu nchini humo uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Maombi hayo ya yaliyofanyika kwa muda wa siku tano yakiongozwa na wachungaji wanaosimamia masuala ya kiroho wa TAUS, Dkt. Christopher Mwashinga Jr na Mch.Israel Kagya yalihusisha hotuba, nyimbo na sala yakiwakutanisha wanachana wa umoja huo kwa njia ya mtandao wa zoom kutoka majimbo 50 ya nchini Marekani wakijikita katika kuombea amani,umoja na mshikamano nchini Tanzania.

Katika moja ya hotuba zake Mch Israel Kagya wa Kanisa la Nations of Praise amewataka watanzania hao kuwa na hali ya utulivu na kuendelea kumwomba MUNGU katika wakati huu mgumu wa majonzi ya kuondokewa na watanzania wenzao, huku Dkt Christopher Mwashinga Jr akiwahimiza kujenga imani ya kuendelea kumtegemea MUNGU zaidi kwani kila jambo liwe zuri ama baya lina mwanzo na mwisho wake duniani.

Kuanzia Oktoba 29 mwaka huu kumeshuhudiwa picha na video mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kutoka Tanzania zikionesha maandamano, watu kupigwa risasi,na kuchomwa moto kwa  miundo mbinu katika maeneo ya Dar es salaam, Mwanza, Arusha na Songwe  ikiwemo vituo vya bus, magari, vituo vya mafuta na watu wengine kupoteza maisha kwa kile kinachoelezwa kupigwa risasi na polisi nchini humo, huku serikali ya Tanzania ikiwa haijatoa idadi kamili ya waliopoteza maisha.

 Kwa mujibu wa taarifa kutoka mashirika ya haki za binadamu ikiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), takriban watu 700 waliuawa ndani ya siku tatu kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi na matokeo ya uchaguzi huo. Vurugu kubwa ziliripotiwa katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, na Arusha, ambapo baadhi ya raia waliripotiwa kuuawa wakiwa majumbani mwao.

Umoja wa Watanzania Waadventista Waishio nchini Marekani na Canada (TAUS) ulianzishwa mwaka 1999 nchini Marekani, na umekuwa ukifanya miradi mbalimbali ikiwemo kujenga makanisa, kusomesha wachungaji, wakunga na kujenga vituo vya afya.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.