MTANGAZAJI

AFRIKA NA WIMBI LA UHALIFU MTANDAONI

 


Barani Afrika, kiwango cha uhalifu wa mtandaoni kimeongezeka kwa kasi ya kutisha katika miaka ya hivi karibuni, hasa kuanzia mwaka 2024 hadi 2025. Ripoti ya hivi karibuni kutoka Shirika la Kimataifa la Polisi ( INTERPOL) imebainisha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya uhalifu unaoripotiwa katika nchi za Afrika Mashariki na Magharibi ni uhalifu wa mtandao. Katika baadhi ya nchi, taarifa za utapeli kupitia mitandao zimeongezeka jambo linaloonyesha kuwa barani Afrika, uhalifu wa kidijitali sasa ni janga linalohitaji hatua za haraka.

Mataifa kama Nigeria, Kenya na Tanzania yameonekana kuwa katika mstari wa mbele, si tu kwa kuwa waathirika wakuu wa uhalifu huu, bali pia kama mifano ya juhudi za kupambana nao. Nigeria kwa mfano, inaongoza kwa visa vya udanganyifu wa utambulisho, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 5.9 ya majaribio ya uthibitishaji wa utambulisho ni ya udanganyifu.

Kwa upande wa Kenya, asilimia 71 ya wananchi waliripoti kuwa wamewahi kulengwa na wadanganyifu wa mtandaoni, ingawa asilimia 11 tu walikubali kupoteza fedha. Nchini Tanzania, kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia za kisasa kama deepfake na synthetic identity fraud, hasa kwa kutumia taarifa bandia zinazotengenezwa kwa msaada wa akili unde (AI).Kwa mujibu wa Operesheni ya INTERPOL iliyofanyika kati ya Septemba na Oktoba 2024, watu1,006 walikamatwa kwa tuhuma za uhalifu wa mtandaoni, na zaidi ya waathiriwa 35,000 waligundulika katika uchunguzi huo. Hasara iliyosababishwa na utapeli huo inakadiriwa kufikia takriban dola milioni 193 za Marekani

Katika baadhi ya visa vilivyorekodiwa nchini Kenya, hivi karibuni watu binafsi waliripoti kupoteza wastani wa shilingi 117,000 za Kenya kwa tukio moja la udanganyifu, sawa na zaidi ya dola 900. Katika sekta ya kifedha, biashara zimekuwa zikipoteza hadi dola 300,000 kwa tukio moja la udanganyifu, hususan linalohusisha hati bandia au wizi wa akaunti.

Ripoti ya Smile ID ya mwaka 2025 inaeleza kuwa kiwango cha udanganyifu unaotumia alama za kibayometriki kilifikia asilimia 25 katika baadhi ya nchi, huku majaribio ya kutumia video au sauti bandia (deepfake) yakiongezeka mara saba ndani ya mwaka mmoja. Hii ni ishara kuwa wadanganyifu sasa wamehamia kwenye matumizi ya teknolojia za hali ya juu ili kufanikisha uhalifu wao.

Katika jitihada za kupambana na changamoto hii, taasisi nyingi za kifedha barani Afrika zimeanza kutumia mifumo ya usalama ya kisasa. Hii ni pamoja na mifumo ya kutambua sura (facial recognition), uthibitisho wa alama za vidole, na matumizi ya akili bandia kugundua shughuli zisizo za kawaida. 

Benki kama Equity Bank,Ecobank na GTBank zimeanzisha kampeni za uelimishaji kwa wateja juu ya usalama wa mitandao. Vilevile, mashirika ya kimataifa ikiwemo INTERPOL na Umoja wa Afrika yameanzisha ushirikiano wa kusaidia nchi wanachama kuboresha sera, miundombinu na mifumo ya ulinzi wa kidijitali.

Licha ya juhudi hizi, ripoti zinaonyesha kuwa takriban asilimia 70 ya nchi za Afrika bado hazina mifumo madhubuti ya kupambana na uhalifu mtandaoni. Hii ni pamoja na uhaba wa sheria mahususi, ukosefu wa hifadhi salama ya data, na uwezo mdogo wa kuchunguza na kushtaki uhalifu wa aina hii.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.