MTANGAZAJI

AHUKUMIWA KULIPA DOLA MILIONI 1.75 KWA KUVUNJA NDOA.

  


Katika tukio linalovuta hisia na mjadala wa kisheria, mahakama ya North Carolina, Marekani  imemhukumu Brenay Kennard, mshawishi maarufu wa TikTok mwenye wafuasi milioni 2.9, kulipa fidia ya dola milioni 1.75 kwa Akira Montague, mke wa zamani wa meneja wake, Tim Montague.

Mahakama ilielezwa kuwa Brenay alihusika moja kwa moja katika kuvunjika kwa ndoa ya meneja wake, Tim Montague, na hivyo kuamriwa kulipa fidia ya jumla ya dola milioni 1.75 kwa Akira Montague, mke wa zamani wa Tim. 

Akira alimshtaki Kennard chini ya sheria ya “alienation of affection,” inayoruhusu mtu kufungua kesi dhidi ya mtu wa tatu anayesababisha mwenzi wake kuacha ndoa. Katika malalamiko yake, Akira alidai kuwa Kennard alijipenyeza katika urafiki wao, akapata taarifa za ndani kuhusu matatizo ya ndoa, ikiwemo usaliti wa Tim wakati wa ujauzito wake, na baadaye kutumia taarifa hizo kumshawishi Tim.

 Ushahidi uliwasilishwa ukionyesha kuwa Kennard na Tim walibadilishana video na jumbe za kimapenzi, walikutana mara kwa mara nyumbani kwa wanandoa hao, na hata walipanga maisha ya baadaye pamoja, ikiwemo kupata watoto wanne hadi watano. 

Akira aligundua uhusiano huo Januari 2024 kupitia video iliyorekodiwa nyumbani kwao. Mahakama ilibaini kuwa Tim alianza kujitenga kihisia na kifedha na mke wake kutokana na ushawishi wa Kennard.

 Uamuzi wa mahakama ulimpata Kennard na hatia ya kushiriki katika “criminal conversation” na kuvunja ndoa, na hivyo kuamuru alipe dola 250,000 kwa kosa la mazungumzo ya kimapenzi na mume wa mtu na dola milioni 1.5 kwa kosa la kuvunja ndoa. 

Kennard amekosoa uamuzi huo, akidai kuwa Akira alimpa ruhusa ya kuwa na uhusiano na Tim, madai ambayo Akira ameyakanusha vikali. Kesi hii imeibua mjadala kuhusu matumizi ya sheria ya “alienation of affection,” ambayo bado ipo katika majimbo machache tu nchini Marekani.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.