UTAPELI MTANDAONI WASHIKA KASI MAREKANI
Watu wazima nchini Marekani wanaendelea kukabiliwa na ongezeko kubwa la matapeli wa mtandaoni, hali ambayo sasa inatajwa kuwa ni tishio la kitaifa.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew Aprili 2025 umebaini kuwa asilimia 73 ya watu wazima Marekani wamewahi kupitia aina fulani ya utapeli au shambulio la mtandaoni kama vile wizi wa taarifa za benki, barua pepe za kitapeli, au akaunti zao kudukuliwa.
Takwimu hizi zinaonesha kuwa vitendo vya uhalifu mtandaoni havichagui umri, kwani vimewaathiri kwa kiwango kikubwa watu wa rika zote — kutoka vijana hadi wazee.
Utafiti huu uliowahusisha watu 9,397 umeeleza kuwa takribani asilimia 48 ya Wamarekani wameshawahi kutozwa fedha isivyo halali kupitia kadi zao za benki au mkopo baada ya kudukuliwa.
Aidha, asilimia 36 walinunua bidhaa mtandaoni ambazo hazikufika au zilikuwa bandia, huku asilimia 29 wakiripoti kuwa akaunti zao binafsi iwe barua pepe, benki au mitandao ya kijamii zilidukuliwa.
Pia, asilimia 24 walikiri kuwa walitoa taarifa zao binafsi baada ya kupokea ujumbe wa kitapeli kupitia simu, ujumbe wa maandishi au barua pepe. Ingawa kwa kiwango kidogo, asilimia 10 walikumbwa na ransomware ambayo ilizuia matumizi ya kompyuta hadi walipolipa fidia, na asilimia 7 waliwekeza kwenye miradi bandia ya mtandaoni.
Kwa ujumla, si jambo la kawaida tena kukumbwa na ujumbe wa kitapeli mara moja moja. Asilimia 68 ya Wamarekani hupokea simu za kitapeli kila wiki, asilimia 63 hupokea barua pepe za udanganyifu, huku asilimia 61 wakikumbwa na ujumbe wa maandishi wa aina hiyo kila wiki. Takribani asilimia 31 hupokea simu za kitapeli kila siku, huku asilimia 28 wakipokea barua pepe na asilimia 20 ujumbe mfupi kila siku.
Ingawa kuna dhana kuwa wazee ndiyo waathirika wakuu, utafiti unaonesha kuwa hali hiyo ni ya kitaifa bila kujali umri. Karibu watu wazima wa rika zote kuanzia wenye miaka chini ya 30 hadi waliopo kwenye kundi la miaka 50 hadi 64 wameripoti kukumbwa na matapeli wa mtandaoni. Hata hivyo, idadi ndogo kidogo ya watu wenye miaka 65 na zaidi (asilimia 66) ndio waliothibitisha kupatwa na visa hivyo.
Tofauti pia zimeonekana kwa misingi ya rangi na kipato. Wamarekani Weusi, Wahispania na Waasia walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kukumbwa na aina tatu au zaidi za matapeli mtandaoni ikilinganishwa na Wazungu.
Kwa upande wa kipato, watu wanaoishi katika familia zenye kipato cha chini waliripoti kwa wingi kuwa wameathirika zaidi – asilimia 26 walisema wamepoteza fedha kutokana na utapeli huu, ikilinganishwa na asilimia 20 ya walioko kipato cha kati na asilimia 15 ya wale wa kipato cha juu.
Katika kiwango cha athari ya kifedha, asilimia 21 ya Wamarekani walipoteza fedha kutokana na utapeli wa mtandaoni, huku vijana wa umri wa miaka 18 hadi 29 wakiongoza kwa kuripoti hasara hizo (asilimia 25), ikilinganishwa na asilimia 15 tu ya wazee. Miongoni mwa waliopoteza fedha, asilimia 30 walikiri kuwa hali hiyo iliwaathiri kwa kiwango kikubwa au cha wastani kifedha, huku wengine wakisema athari hizo zilikuwa ndogo au hazikuwepo kabisa.
Jambo la kusikitisha ni kwamba asilimia 74 ya waathirika wa kifedha hawakuripoti kwa vyombo vya sheria, labda kwa hofu au kukata tamaa ya kupata msaada. Ni asilimia 26 tu waliowahi kuripoti, ambapo walioathiriwa zaidi kifedha ndio waliokuwa na uwezekano mkubwa wa kutoa taarifa. Asilimia 42 ya waliopata hasara kubwa kifedha waliripoti kwa vyombo vya sheria, ikilinganishwa na asilimia 24 waliopata athari za wastani, na asilimia 16 tu waliopata madhara madogo au hakuna kabisa.
Kwa ujumla, matokeo haya yanaonesha kwamba utapeli wa mtandaoni umefikia kiwango cha hatari, na unahitaji hatua za haraka kutoka kwa serikali, Kampuni za teknolojia, taasisi za fedha, na jamii kwa ujumla. Huku dola bilioni 16.6 zikipotea kwa uhalifu wa mtandaoni mwaka 2024 pekee, ujumbe kwa umma ni mmoja tu: kuwa makini, tambua viashiria vya utapeli, na ripoti mara moja unapodhani umetapeliwa.
Post a Comment