HOFU YA WATANZANIA WALIOKO MAREKANI KUWEKEZA NYUMBANI.
Idadi ya Watanzania walioko nchini Marekani imeendelea kuongezeka na kufikia takribani Watanzania 100,000, kwa mujibu wa takwimu za makadirio ya Diaspora ya mwaka 2024 kutoka Ubalozi wa Tanzania Washington D.C. Idadi hiyo ni pamoja na wanafunzi, wafanyakazi wa taaluma mbalimbali, wafanyabiashara, na wale waliopata uraia wa Marekani.
Ingawa miongoni mwao wana uwezo mkubwa wa kifedha na ujuzi, bado wanaonesha wasiwasi mkubwa wa kuwekeza Tanzania kutokana na changamoto mbalimbali za kisheria na kiutendaji.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa kwa baadhi ya watanzania waishio katika jiji la Houston,Texas linaloelezwa kuwa na watanzania walio wengi zaidi nchini Marekani unaonesha kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazowatisha kuwekeza ni kutokuwepo kwa uraia pacha kwa watu wazima. Sheria ya sasa ya Tanzania inawazuia waliopata uraia wa nchi nyingine kumiliki ardhi au kuendesha shughuli za kibiashara kwa jina lao, jambo linalowalazimu kutumia majina ya ndugu au marafiki, hali inayosababisha udanganyifu na migogoro ya mali.
Zaidi ya hapo, wengi wanalalamikia urasimu mkubwa katika baadhi ya taasisi za umma, ambapo huduma kama usajili wa kampuni, upatikanaji wa vibali vya ujenzi au ardhi huchukua muda mrefu na mara nyingine huhitaji kutoa rushwa ili kusukuma mambo mbele.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashirika kadhaa ya Watanzania waishio Marekani, zaidi ya asilimia 60 ya wahamiaji waliowahi kuwekeza nyumbani wameripoti kupoteza fedha au mali kutokana na usimamizi mbovu, hasa kwa kuamini ndugu,marafiki na mawakala wasiokuwa waaminifu. Wengine wamepoteza hamu kabisa ya kuwekeza Tanzania baada ya kushindwa kupata haki kupitia mfumo wa mahakama au taasisi za serikali.
Pia, mabadiliko ya mara kwa mara ya sera, pamoja na hofu ya kukosekana kwa utulivu wa kisiasa au kiuchumi, huongeza mashaka kwa wahamiaji hawa. Wengi wao hulazimika kuahirisha uwekezaji hadi pale watakapoona hali imeimarika au sheria zimefanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wa Diaspora wanasema kuwa kama serikali ya Tanzania itaruhusu uraia pacha kwa watu wazima kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, basi sehemu kubwa ya hao Watanzania takribani 100,000 walioko Marekani wanaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia mitaji, ujuzi na mtandao wao wa kimataifa.
Kwa sasa, Watanzania waishio Marekani wanaendelea kuomba marekebisho ya sheria na kuboreshwa kwa mifumo ya huduma serikalini ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuijenga Tanzania yao, hata wakiwa mbali na nyumbani.
Post a Comment