MTANGAZAJI

SHEMASI WA KANISA APEWA ZAWADI YA GARI BAADA YA USHUJAA



Katika mji wa Wayne, Michigan,Marekani shemasi mmoja wa kanisa amepongezwa kwa ushujaa wake baada ya kumzuia mshambuliaji aliyekuwa na silaha nzito kuingia ndani ya ibada ya Jumapili. 

Richard Pryor, shemasi wa Kanisa la CrossPointe Community alitumia gari lake aina ya Ford F-150 ya mwaka 2018 kumgonga mshambuliaji huyo, aliyekuwa amevaa fulana ya kivita na kubeba bunduki pamoja na bastola. 

Tukio hilo lilitokea 22 Juni,2025 wakati waumini zaidi ya mia moja, wakiwemo watoto waliokuwa wakihudhuria shule ya Biblia wakati wa likizo, walikuwa ndani ya kanisa hilo.

Mshambuliaji huyo, aliyejitambulisha baadaye kama Brian Browning mwenye umri wa miaka 31, alifyatua risasi na kumjeruhi mtu mmoja mguuni kabla ya kuuawa na walinzi wa usalama wa kanisa. 

Pryor, ambaye hakuwa na silaha wakati wa tukio hilo, alisema alitambua hakuwa na muda wa kusubiri msaada, na hivyo akaamua kutumia gari lake kama njia ya kuzuia janga kubwa. “Nikatambua hakuna muda tena. Nilichofanya ni kumgonga, na naamini hiyo ilikuwa ni kazi ya Bwana,” alisema Pryor.

Kwa kutambua ushujaa huo, kampuni ya magari ya Jack Demmer Ford imemzawadia Pryor gari jipya aina ya Ford F-150 ya mwaka 2025 yenye thamani ya takriban dola 70,000. 

Gari hilo limetolewa kwa mkataba wa miaka miwili. Mmiliki wa kampuni hiyo, Matthew Demmer, amesema hatua hiyo ni njia ya kuthamini ujasiri wa Pryor ambaye aliokoa maisha ya wengi. “Angeweza kupoteza maisha yake kwa ajili ya wengine. Hii ilikuwa njia bora ya kurudisha shukrani,” alisema Demmer.

Mchungaji wa kanisa hilo, Bobby Kelly, amesema alikuwa amewahi kukutana na mshambuliaji huyo mara tatu kabla ya tukio, lakini hakuwahi kutishiwa. Kelly alisema Browning alikuwa akipambana na changamoto za afya ya akili na kuamini alikuwa anasikia sauti za Mungu. Mama wa mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa akihudhuria kanisani mara kwa mara, hakuwapo siku ya tukio hilo. 

Mchungaji Kelly alimwelezea Pryor kama shujaa wa kweli na kusema hatua yake ilisaidia walinzi wa usalama kuchukua hatua kwa haraka na kuzuia maafa makubwa.

Shukrani na pongezi zimeendelea kutolewa kwa Pryor kutoka kwa waumini na jamii kwa ujumla, huku wengi wakimshukuru Mungu kwamba, licha ya taharuki kubwa, maisha ya watu wengi yaliokolewa. 

Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea, huku viongozi wa kanisa wakisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika huduma za afya ya akili kwa ajili ya kuzuia matukio kama haya siku zijazo.



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.