TAKWIMU ZAONYESHA KUPUNGUA KWA WAADVENTISTA DUNIANI
Pamoja na mafanikio katika kupeleka injili na kuenea kwa ujumbe wa Kanisa la Waadventista wa Sabato duniani, kupungua kwa idadi ya waumini waliobatizwa katika kanisa hilo linaendelea kuwa suala nyeti linalohitaji uangalizi wa haraka.
Kanisa la Waadventista wa Sabato limeendelea kukua kwa kasi duniani, likifikia jumla ya waumini milioni 23.684 mwishoni mwa mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti rasmi ya Idara ya Takwimu na Utafiti ya Makao Makuu ya Kanisa hilo (ASTR).
Hili ni ongezeko kutoka milioni 16.92 mwaka 2015, likiwa ni ushahidi wa mafanikio ya utume wa kanisa hilo ulimwenguni. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Kanisa la Waadventista wa Sabato linakabiliwa na changamoto ya upotevu wa waumini wake.
Kwa mujibu wa ASTR kati ya watu 47,005,367 waliobatizwa na kujiunga na Kanisa tangu mwaka 1965, watu 20,290,098 wanaonekana kutoka kwenye ushirika wa Kanisa kufikia Desemba 2024, hali inayowakilisha asilimia 43.17 ya waliojiunga.
Hii ina maana kuwa kwa kila waumini 100 wanaojiunga, takribani 43 huacha Kanisa.
Ripoti ya mwaka 2023 pekee inaonyesha kuwa waumini 836,905 waliondolewa kwenye rekodi kutokana na kutoonekana au kujiondoa rasmi, kiwango ambacho ni miongoni mwa vya juu zaidi katika historia ya karibuni ya Kanisa.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Idara inayohusika na Malezi,Kukuza na Kudumisha Ushirika wa Waumini ya Kanisa la Waadventist wa Sabato, sababu kuu za waumini kuondoka hazihusiani moja kwa moja na mafundisho ya Kanisa, bali zinatokana na changamoto za kijamii ikiwemo ukosefu wa marafiki wa karibu ndani ya Kanisa, migogoro na viongozi au waumini wengine, na kutopata msaada wa kiroho au kihisia wakati wa changamoto za maisha.
Utafiti huo unaonesha kuwa waumini wapya wana uwezekano mkubwa wa kubaki ikiwa watapata angalau marafiki sita wa karibu ndani ya jumuiya ya waamini.
Ripoti hiz0, zilizochapishwa rasmi April 8, 2025 kwenye tovuti ya Takwimu na Utafiti ya Makao Makuu ya Kanisa hilo (ASTR) , zinaonyesha hitaji kubwa la Kanisa kuimarisha huduma ya ufuatiliaji, malezi ya kiroho, na kukuza mazingira ya upendo wa kindugu ili kuhakikisha wale wanaoingia katika imani wanadumu na kukua katika Kristo.
Kanisa la Waadventista wa Sabato linatambulika kuwa na waumini wengi duniani katika nchi za Brazil na Zambia, zikiwa mbele ya mataifa mengine. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, Brazil ina waumini zaidi ya 1.8 milioni. Zambia inafuata kwa idadi ya waumini zaidi ya 1.46 milioni. Nchi nyingine zenye waumini wengi waadventista ni India na Uphilipino.
Kupungua kwa waumini ni suala la kiroho, kijamii na kimkakati ambapo inahitaji mwitikio wa pamoja wa viongozi, wachungaji, na washiriki wa kawaida. Kupitia maombi, mawasiliano ya karibu, na kujenga mazingira yenye upendo wa kweli wa kikristo, kanisa linaweza kugeuza hali hii na kuimarisha ushirika wa kudumu kati ya washiriki wake.
Post a Comment