MCHUNGAJI NDA KUTOKA CAMEROON ATWAA TUZO YA UONGOZI WA KIROHO
Jioni ya Julai 6, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano jijini St. Louis, Umoja wa Wanawake Waadventista (AAW) uliandaa hafla ya tuko ya mwanamke wa mwaka. Tukio hilo lilikuwa ni kusherehekea na kutambua wanawake waliotoa mchango mkubwa katika huduma, sayansi, tiba, na elimu.
Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa wamisionari, wasomi, na viongozi wa fikra waliotafiti kwa kina nafasi na mchango wa wanawake katika Biblia na jamii. Wote walikusanyika kwa imani moja kwamba wanawake wana haki sawa katika kanisa, huduma na maisha ya kijamii.
Katika tukio hilo, Anathasie Nda aliandika historia kwa kutambuliwa rasmi kutokana na mchango wake mkubwa katika huduma ya kichungaji. Nda ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Mchungaji nchini Cameroon, na mmoja wa wanawake wa kwanza barani Afrika kubatiza waumini.
Amezaliwa katika familia ya Kikatoliki huko Esse, Cameroon, lakini baada ya kufunga ndoa na Mwadventista, alibadilika na kujiunga na imani ya Waadventista mnamo 1974. Alisomea thiolojia katika Seminari ya Waadventista ya Nanga Eboka, na kuwa mwanamke wa kwanza kufanya hivyo katika Union ya Afrika ya Kati ya Kanisa la Waadventista.
Huduma yake ilikua licha ya upinzani, na badala ya watu 30 waliotarajiwa kubatizwa, zaidi ya watu 300 walibatizwa kupitia kazi yake. Katika kipindi cha miaka 10, alianzisha makanisa kumi, na mara nyingi alitembea zaidi ya maili 30 kila Sabato ili kuwahudumia waumini wake. Baadaye, alihudumu kwa nafasi ya uchungaji katika shule ya Maranatha kwa miaka mitano, ambako aliwafikia wanafunzi na makundi yaliyosahaulika, ikiwemo watoto wa mitaani na watu wenye ukoma.
Mwaka 1993, Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (GC) ilimtambua rasmi kuwa “mwanamke mwenye bidii na kujitolea zaidi katika kazi ya Mungu duniani kote.” Baada ya kupokea tuzo yake, alieleza furaha yake kwa kurukaruka kwa shangwe mbele ya wahudhuriaji, huku ukumbi mzima ukimshangilia.
Post a Comment