MTANGAZAJI

MAKAMU WA KIONGOZI WA KANISA LA WAADVENTISTA ULIMWENGUNI

 


Julai 6, 2025, wajumbe wa Mkutano wa 62 wa Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (GC) uliofanyika St. Louis, Missouri, waliwachagua makamu saba wa Kiongozi wa Kanisa hilo kwa kipindi cha miaka mitano (2025–2030). Kura ya uteuzi ilipitishwa kwa kura 1,798 za ndio  dhidi ya 92.

Makamu walioteuliwa ni: (Kutoka kulia kwenye picha)

  • Thomas L. Lemon - Ambaye alianza uchungaji huko Maryland na Texas, kabla ya kuhamia kwenye nafasi za uongozi. Amewahi kuwa msaidizi wa Kiongozi wa Konferensi ya Rocky Mountain, Mkurugenzi msaidizi wa Chama cha Wachungaji huko Oregon (2002-2006), na Mwenyekiti wa Konferensi ya Minnesota (2006-2009) pamoja na Unioni Konferensi ya Kati mwa Amerika. Ana shahada ya kwanza ya thiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Waadventista cha Southwestern na Shahada ya Uzamili ya Uungu  kutoka Seminari ya Thiolojia ya Chuo Kikuu cha Andrews.
  • Audrey E. Andersson -  Mwenye shahada ya uzamili katika huduma ya uchungaji, alizaliwa Ireland na kukulia katika familia ya mchungaji, Alipata shahada ya kwanza ya theolojia kutoka Chuo cha Newbold nchini Uingereza, kisha katika  taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma. Baada ya kufanya kazi ya Uhariri wa Kisheria wa Estates Gazette na kuanzisha kampuni ya ushauri ya Mawasiliano nchini Uswidi, mwaka 2010 aliteuliwa kuwa Katibu wa Divisheni ya Trans-Europe. Anaendelea na wadhifa huu ikiwa ni mara yake ya pili kuchaguliwa, mara ya kwanza ilikuwa Juni 2022. 

    Pierre E. Omeler - Mzaliwa wa Haiti ambaye hivi karibuni alikuwa ni Kiongozi wa Unioni Konferensi ya Atlantiki katika Divisheni ya Kaskazini mwa Amerika. Kabla ya hapo, alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya Konferensi ya Kaskazini-Mashariki, zikiwemo Katibu, Makamu wa Mwenyekiti, Mkurugenzi wa Huduma. Omeler alipata shahada ya kwanza ya Thiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Oakwood, Shahada ya Uzamili ya Uungu kutoka Chuo Kikuu cha Andrews, na Shahada ya Uzamivu ya Huduma ya Kichungaji kutoka United Theological Seminary na anafahamu vyema lugha ya Kifaransa

  • Artur A. SteleAlizaliwa Januari 30,1961, Kaskelen , Kazakhstan, alianza taaluma yake katika fani ya famasia kabla ya kuingia katika huduma ya kichungaji. Alipata shahada ya thiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Friedensau nchini Ujerumani mwaka 1986, kisha shahada ya uzamili na uzamivu katika thiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Andrews mnamo 1993 na 1996. Stele ambaye alishawahi kuchaguliwa katika nafasi hii mwaka 2010 ameshashika nafasi ya Ukuu wa masomo na Rais wa Seminari ya Theolojia ya Zaoksky nchini Urusi, na baadaye Mwenyekiti wa Divisheni ya Ulaya -Asia. Anauwezo wa kuzungumza Kirusi, Kijerumani, na Kiingereza.

  • Saw Samuel Akitokea Myanmar, kabla ya uteuzi huu, Saw Samuel alikuwa ni katibu msaidizi wa Konferensi Kuu, ambapo alikuwa mwakilishi kwa Divisheni za Asia-Pasifiki Kaskazini, Asia-Pasifiki Kusini, Asia Kusini, na Afrika ya Magharibi-Kati. Amewahi kuhudumu nchini Thailand na Ufilipino, ana shahada ya kwanza kutoka Chuo cha Spicer Memorial nchini India, Shahada ya Sanaa ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Andrews nchini Marekani, na Shahada ya Udaktari wa Huduma ya Kichungaji kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Waadventista ya Mafunzo ya Juu (AIIAS) nchini Ufilipino.

  • Leonard A. Johnson - Amehudumu kwa zaidi ya miongo minne katika nafasi za kichungaji na kiutawala. Tangu mwaka 2018, amekuwa Katibu wa Divisheni ya Inter-America. Kabla ya hapo, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Unioni ya Atlantic Caribbean (2010–2018) na Konferensi ya Bahamas (2003–2010), pamoja na kuwa Katibu wa Konferensi hiyo. Johnson ana shahada ya kwanza ya thiolojia, shahada ya uzamili ya dini, na shahada ya udaktari wa huduma ya kichungaji. Mwaka 2017, alitunukiwa tuzo ya heshima ya Companion of the Most Distinguished Order of Saint Michael and Saint George (CMG) . Ni moja ya tuzo za kifalme zinazotolewa na familia ya kifalme ya Uingereza kwa watu waliotoa mchango mkubwa katika huduma za kimataifa, hasa katika nchi za Jumuiya ya Madola au katika masuala ya Diplomasia na Uongozi wa umma

  • Robert Osei-Bonsu Mzaliwa wa Ghana, alikuwa Kiongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika  Divisheni ya Afrika ya Magharibi-Kati (WAD), ambako aliongoza mpango wa uinjilisti wa Impact 2025 uliolenga kuimarisha kazi ya utume na kukuza ukuaji wa kanisa katika eneo hilo. Kabla ya hapo, alishikilia nyadhifa za uongozi katika  kanisa na elimu, ikiwa ni pamoja na kuwa Rais na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Valley View nchini Ghana, na Mkuu wa seminari ya thiolojia ya Chuo Kikuu cha Waadventista cha Afrika kilichoko Kenya. Osei-Bonsu amewahi kuwa mchungaji Afrika na Ulaya, ikiwa ni pamoja na kuwa Mchungaji kiongozi katika Konferensi ya Kusini mwa Uingereza. Anaheshimika sana kwa uwezo wake wa kulea viongozi, kushirikiana na jamii, na mchango wake mkubwa katika elimu ya thiolojia.

    Ana shahada ya kwanza katika masomo ya thiolojia, shahada mbili za uzamili, moja katika theolojia ya Biblia na nyingine katika uongozi wa elimu, pamoja na shahada ya uzamivu katika masomo ya kihistoria ya theolojia.

 Miongoni mwa ajukumu yao yatakuwa ni kusaidia uratibu wa utawala wa kimataifa, kuwaelekeza viongozi katika kila Divisheni 13 za kanisa hilo na kuendeleza mipango mikakati ya huduma ya kanisa.

Uchaguzi huu ni sehemu ya mchakato mpana wa uteuzi unaofanyika wakati wa Mkutano huu Mkuu wa mwaka 2025 tukio la kila baada ya miaka mitano linalowaleta pamoja wajumbe kutoka duniani kote kwa maamuzi muhimu, ibada ya pamoja, na maombi ya kuombea mwelekeo wa siku zijazo wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.