KATIBU MKUU MPYA WA WAADVENTISTA WA ULIMWENGUNI
Richard E. McEdward amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni. Wajumbe walimpigia kura McEdward katika Mkutano Mkuu wa 62 wa Konferensi Kuu (GC) unaofanyika St. Louis, Missouri.
Akiwa mmoja wa maafisa watatu wakuu wa uongozi wa kanisa hilo lenye zaidi ya waumini milioni 23 katika zaidi ya nchi 200, McEdward atasimamia uratibu wa shughuli za kimataifa za kanisa hilo. Majukumu yake yanajumuisha kusaidia miundo ya utawala, kuongoza mabadiliko ya uongozi, na kuwezesha taasisi za kanisa kutekeleza huduma yao kwa ufanisi katika maeneo na tamaduni mbalimbali.
Jina la McEdward liliwasilishwa na Kamati ya Uteuzi ya Mkutano Mkuu na uteuzi wake uliwasilishwa kwa wajumbe wote na kuthibitishwa kwa kura kutoka kwa wajumbe waliowakilisha kila eneo la kanisa duniani ambapo kura za kuthibitisha jina lake zilikuwa 1,630 za ndio dhidi ya 153.
Kabla ya kuchaguliwa, alikuwa ni Kiongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Unioni Misheni ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini (MENAUM), ambako aliongoza juhudi za kimkakati katika moja ya maeneo magumu zaidi kwa huduma ya injili duniani.
McEdward ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa 25 katika historia ya kanisa hilo alizaliwa Seattle, Washington, na alitumia miaka ya utotoni Jeddah, Saudi Arabia, ambako familia yake iliishi kama wageni. Uzoefu huo wa awali wa kuishi kati ya jamii mbalimbali unaelezwa kuwa ulimjengea huruma ya kina na kusudi la kushiriki upendo wa Kristo katika mipaka ya kitamaduni na kidini.
Ana shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Walla Walla, Shahada ya Uzamili ya Uungu kutoka Chuo Kikuu cha Andrews, na Shahada ya Uzamivu ya Uinjilisti wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Theolojia cha Fuller. Huduma yake ya kikazi inajumuisha kuwa mchungaji, Mratibu wa uanzishaji wa makanisa huko Sri Lanka na Divisheni ya Asia-Pasifiki Kusini, na Mkurugenzi msaidizi wa Taasisi ya Utume wa Ulimwenguni ya Chuo Kikuu cha Andrews.
Baadaye alijiunga na Konferensi Kuu (GC), ambako alihudumu kama Mkurugenzi msaidizi wa Ofisi ya Utume wa Waadventista na Mkurugenzi wa Vituo vya Utume wa Duniani kwa Dini mbalimbali. Mwaka 2016, alichaguliwa kuongoza MENAUM, makao yake yakiwa Beirut, Lebanon, ambako alisaidia wafanyakazi wa utume na kupanua uwepo wa utume wa kanisa hilo katika maeneo ya mijini na yasiyofikiwa.
McEdward amemuoa Marcia McEdward, muuguzi wa aliyesajiliwa, Wana watoto wawili wakubwa, Julia na Joshua.
Katibu Mkuu wa Kanisa hilo ulimwenguni ana jukumu muhimu katika uratibu wa kimataifa wa Kanisa la Waadventista wa Sabato. Likihusisha kusimamia shughuli za kiutawala, kusaidia mabadiliko ya uongozi, kudumisha kumbukumbu sahihi za uanachama na sera, na kuwaongoza viongozi wa kikanda katika kupanga na kutekeleza utume. Pia hufanya kazi kwa karibu na idara zinazolenga utume, zikiwemo Ofisi ya Utume wa Waadventista, Taasisi ya Utume wa Dunia, na Ofisi ya Kumbukumbu, Takwimu, na Utafiti
Post a Comment