MWENDESHA MASHTAKA AAMURU MCH MACKENZIE NA WENZAKE WASHITAKIWE
Mwendesha mashtaka Mkuu wa Kenya Jumanne ya Januari 16 mwaka huu aliamuru watu 95 wanaotuhumiwa kuongoza Kanisa linalodaiwa kuendesha ibada ya maangamizi washitakiwe kwa mauaji, ukatili, kutesa watoto na uhalifu mwingine katika vifo vya watu 429 wanaoaminika kuwa waumini wa kanisa hilo.
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Kenya , Mulele Ingonga, alikuwa akijibu shinikizo kutoka kwa hakimu katika Kaunti ya Pwani ya Kilifi ambaye aliueleza upande wa mashtaka kuwafungulia mashtaka washukiwa ndani ya majuma mawili la sivyo mahakama itawaachilia.
Kwa miezi kadhaa tangu kukamatwa kwa watu hao Aprili mwaka jana, waendesha mashtaka walikuwa wameiomba mahakama ruhusa ya kuendelea kumshikilia kiongozi wa kanisa hilo Paul Mackenzie na wengine 28 huku wakichunguza kesi iliyowashtua Wakenya kwa kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki na madai ya njaa na kunyongwa.
Hakimu Mkuu Yousuf Shikanda alikataa ombi la hivi punde la kuwashikilia washukiwa hao kwa siku 60 zaidi, akisema upande wa mashtaka umepewa muda wa kutosha kukamilisha upelelezi.
Post a Comment