MTANGAZAJI

TANZANIA NA MCHAKATO WA MFUMO WA KUWAFIKIA DIASPORA

  


 Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi James Bwana ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imejidhatiti kufanya maboresho ya mifumo ya Tehama katika sekta za umma na sekta binafsi ili kuhakikisha fursa mbalimbali zinazopatikana nchini zinawafikia diaspora kwa wakati. 

Hayo yameelezwa katika siku ya pili ya mkutano wa wadau wa sekta za umma na binafsi uliojadili masuala mbalimbali kuhusu ushiriki wa Diaspora katika shughuli za maendeleo ya Taifa uliomalizika leo tarehe 27 Desemba 2022 Jijini Dodoma. 

Miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa na wadau kwa ajili ya maboresho ni pamoja na: kuongeza kazi ya ukamilishwaji wa mapendekezo ya kupatikana kwa hadhi maalum kwa Diaspora, Uandaaji na ukamilishaji wa Sera na sheria ya Diaspora ya Tanzania, taasisi za fedha kuwa na huduma rafiki na zenye riba nafuu kwa Diaspora na ukamilishaji wa mfumo wa kidigitali wa kuhifadhi taarifa muhimu za watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, ujulikanao kama “Diaspora Digital Hub”. Mfumo huu utawezesha kuwatambua Diaspora na mahitaji yao pamoja na kuongeza ubunifu katika utoaji huduma

 Maeneo mengine ni uharakishwaji wa mchakato wa kuwapatia Diaspora vitambulisho vya Taifa, kuwepo kwa siku maalum ya Diaspora ili kuwajengea uzalendo, Balozi za Tanzania nje ya nchi kusimamia kwa karibu changamoto mbalimbali za Diaspora, wadau kuwekeza zaidi katika kupata uzoefu kutoka mataifa mengine yaliyofanikiwa katika masula ya Diaspora, maboresho katika taratibu na sheria za ununuzi na umiliki wa ardhi na majengo, kuanzishwa kwa madawati maalum yanayohudumia Diaspora katika sekta za Umma na Binafsi hususan huduma za kidigitali.

 Akifunga mkutano huo Naibu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Diaspora, Ofisi ya Rais – Ikulu Zanzibar, Bi. Maryam Ramadhan Hamoud amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano na uzoefu wake katika hatua mbalimbali za uandaji wa sera na sheria ya Diaspora kwa upande wa Tanzania bara kwa kuwa tayari Tanzania-Zanzibar ilishakamilisha taratibu hizo. 

Hata hivyo baadhi ya Diaspora wa Tanzania  kutoka nchi mbalimbali Duniani wamekuwa wakieleza kuwa hawakubaliani na pendekezo la Tanzania kuwapatia kwa hadhi maalum bali wanataka uraia pacha kama ilivyo kwa Diaspora wa nchi zingine za Afrika ya Mashariki.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.