MTANGAZAJI

DIASPORA WATAKIWA KUITANGAZA TANZANIA

 


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wana-Diaspora wote kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kokote waliko na wawe tayari kuainisha fursa zilizopo nchini Tanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa  ambaye yuko Tokyo, Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa wito huo  Septemba 28, 2022 alipokutana na wanachama wa Tanzanite ambayo ni Jumuiya ya Watanzania waishio Japan kwenye hoteli ya Ana Intercontinental jijini humo. Jumuiya hiyo ina wanachama ambao ni wafanyakazi, waliojiajiri na wanafunzi.
Amewataka watambue fursa zilizopo nchini Tanzania  na kuzisemea vizuri ili iwe fursa ya kupata wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na ikibidi wafanye ubia na Watanzania.
Amewataka pia watumie Kiswahili kama njia ya kukuza ajira kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka kwenye mitaala yao.
Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwaeleza mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo uboreshaji katika sekta za elimu, afya, maji, nishati, usafiri na usafirishaji na miundombinu ya barabara na reli.
Akitoa mfano kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi, Serikali imejenga miradi mikubwa ya maji katika miji ya Bunda, Butiama, Bukoba, Tarime, Rorya ambayo yote inatumia maji ya Ziwa Victoria.
Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha barabara kuu za kuunganisha mikoa isipokuwa barabara mbili tu. “Tunaendelea kuunganisha wilaya kwa wilaya na tumeanzisha TARURA ili kuimarisha barabara za vijijini ambapo kwenye kila makao makuu ya wilaya wanapatiwa kilometa mbili za barabara ya lami.”

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.