TANZANIA NA ITALIA KUONGEZA NGUVU SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJ
Tanzania na Italia
zimeahidi kushirikiana kukuza na kuendeleza sekta ya biashara ya
uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Akihutubia
sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Italia,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Liberata Mulamula alisema Tanzania imeboresha mazingira ya biashara
na uwekezaji na kuwasihi wafanyabiashara wa Italia kuja kuwekeza nchini
kwa kuwa ni salama zaidi.
“Natumia
fursa hii kuwahakikishia ushirikiano wetu wa kukuza na kuendeleza
biashara na uwekezaji nchini, Serikali imechukua jitihada mbalimbali za
kuwavutia wawekezaji kuwekeza hapa nchini ikiwemo kuondoa vikwazo vya
biashara,” alisema Balozi Mulamula.
Balozi
Mulamula aliongeza kuwa, Tanzania na Italia zimekuwa na utamaduni wa
kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia majukwaa mbalimbali
ya biashara na matokeo chanya ya majukwaa hayo yameanza kuonekana ambapo
Disemba, 2021 kupitia kongamano la biashara na uwekezaji lililofanyika
Italia, kampuni ya Kiitaliano ‘Suness Limited’ inayojishughulisha na
uchimbaji wa madini ilisaini makubaliano na Shirika la Taifa la madini
(Stamico) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa shaba inayopatikana
Kilimanjaro.
“Ni
Imani yangu kuwa kupitia kongamano la biashara na uwekezaji
litakalofanyika mwezi Septemba 2022 Jijini Dar es Salaam na Zanzibar
litatoa fursa nyingi zaidi kwa pande zote mbili kuchangamkia fursa
zinazopatikana kwenye sekta za kilimo, viwanda, miundombinu, elimu,
utalii na uchumi wa buluu,” alisema Balozi Mulamula
Pamoja
na mambo mengine, Balozi Mulamula aliishukuru Serikali ya Italia kwa
ushirikiano imara wa kuchangia maendeleo ya Tanzania ambapo wiki ijayo
Tanzania na Italia zitasaini makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu wa
Euro milioni 20 kwa ajili ya kuboresha elimu ya ufundi katika mikoa ya
Mbeya, Arusha, mwanza, Songwe, Zanzibar na Dar es Salaam.
Kwa
upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania ,Marco Lombardi ameipongeza
Tanzania kwa jitihada kubwa za kuboresha na kuimarisha mazingira ya
biashara nchini.
“Kwa
kweli tunafurahishwa sana na namna mazingira ya biashara
yanavyoboreshwa hapa Tanzania, kwa kweli tutaendelea kuwashawishi
wafanyabiashara wetu waje kuwekeza hapa kwani ni sehemu salama uya
kuwekeza,” alisema Balozi Lombardi
Aliongeza
kuwa kitendo cha Tanzania kuviondoa vikwazo vya biashara kimeongeza
imani kubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengi duniani kuiona
Tanzania ni salama. Aidha, Balozi Lombard alimpongeza Rais wa Jamahuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya
kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na mataifa mengine duniani.
“Napenda
kuwahakikishia kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo baina yetu kwa maslahi mapana ya
pande zote mbili,” aliongeza Balozi Lombardi.
Tanzania
na Italia zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja za kilimo, afya, elimu,
maji, nishati, utalii na maendeleo ya sekta binafsi.
Post a Comment