MTANGAZAJI

TANZANIA YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA KILIMO ITALIA

 

Tanzania kwa mara ya kwanza imeshiriki katika maonesho ya kimataifa ya kilimo yanayojulikana kama MACFRUT FIERA yanayoendelea mjini Rimini, nchini Italia.

Maonesho hayo yanawakutanisha wazalishaji,wanunuzi na wauzaji wa bidhaa za kilimo cha mbogamboga na matunda, ufugaji wa kuku na mashine za kisasa zinazotumika katika kilimo.

Akifungua maonesho hayo, Waziri wa Kilimo wa Italia,Stefano Patuanelli, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na
matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji na usalama wa chakula.

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo umevutia ushiriki wa sekta binafsi katika maonesho hayo ambayo tunda la mwaka huu
ni parachichi.

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, aliwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya kilimo na sekta nyinginezo.

“Nawahakikishia kuwa Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza kero zilizokuwa hapo awali na kwamba, Watanzania wapo
tayari kuwapokea,” alisema Balozi Kombo.

Maonesho ya MACFRUT hufanyika kila mwaka. Awamu inayofuata ya maonesho (MACFRUT FIERA2023) itafanyika mwezi Mei, 2023 katika mji wa Rimini.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.