MTANGAZAJI

WATANZANIA WAHIMIZWA KUSHIRIKI SENSA

 

Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania Agosti 23, 2022 ikiwa na sura tofauti kiutendaji ikilinganishwa na Sensa zilizopita na serikali ya nchi hiyo ikitarajia kuwa na mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na taifa hilo kwa ujumla.

 Imeelezwa kuwa katika sensa ya mwaka huu, taarifa zitakukusanywa kwa kutumia vifaa vya kisasa tumizi (vishikwambi) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi kwa wakati za taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa ambapo kila mmoja atahesabiwa mara moja tu.

 Serikali ya Tanzania imekuwa ikieleza kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kushiriki na kutimize wajibu wake kufanikisha zoezi hilo la kitaifa ili kupata taarifa na takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi na watu wake kulingana na idadi ya watu na eneo husika kwa msingi wa ugawaji wa rasilimali ya taifa kwa kila eneo la utawala  nchini humo..

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan wakati anazindua rasmi wa Nembo ya Sensa Watu na Makazi Aprili 08, 2022 mjini Zanzibar na kutangaza zoezi hilo kufanyika  Jumanne Agosti 23, 2022, aliwahimiza Watanzania kujitokeza siku hiyo kushiriki zoezi hilo adhimu kwa nchi ili kuwezesha taifa kupata taarifa na takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kiuchumi na kijamii.

 Taarifa hizo ni nyenzo msingi kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania  ya mwaka 2025 inayolenga kuleta mageuzi makubwa nchini humo  katika sekta za afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

 Kutokana na umuhimu wa Sensa kwa taifa, Rais Samia anazihimiza taasisi za Serikali na binafsi kutumia Nembo Sensa katika shughuli zote za kiserikali na za sekta binafsi ili kuitangaza Sensa hadi itakapokamilika.

Zoezi hilo hufanyika Tanzania kila baada ya miaka 10 ili kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao ili kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo ya nchi kulingana na uhitaji na mazingira ya watanzania waliyopo.

 Ili kukamilisha zoezi la Sensa, ni muhimu watu wote watakaolala katika kaya binafsi usiku wa kuamkia siku ya Sensa pamoja na watu wote watakaokuwa katika kaya za jumuiya zikiwemo hoteli, nyumba za kulala wageni, hospitalini, magereza, mabweni ya wanafunzi, kambi za kijeshi, vituo vya kulelea watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo yatima na wazee, kambi za wavuvi na watu wasio na makazi maalum kushiriki sensa hiyo.

 Vituo vya usafiri wa umma vikiwemo vituo vya mabasi, garimoshi, viwanja vya ndege na bandari navyo ni eneo jingine ambalo litahusisha zoezi la sensa. Katika maeneo hayo, watu watahesabiwa kwa utaratibu maalum utakaoandaliwa na Kamati za Sensa katika ngazi za mitaa, kitongoji na Shehia.

 Akizungumza katika kikao cha Maofisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikalini kinachofanyika Mei 12, 2022 jijini Tanga, Kamisaa wa Sensa nchini Tanzania na Spika Mstaafu Anne Makinda amesema sensa ni muhimu kwa nchi, suala la rushwa halina nafasi katika kukamilisha zoezi hilo, hivyo, ni kosa kisheria kuwaomba pesa makarani ambao watafanyakazi ya zoezi hilo.

 "Ni marufuku kutoa pesa, kisa kazi ya ukarani, acheni tabia hiyo na nyie waombaji msishawishike kutoa pesa kwa mtu yeyote kwa kuwa maombi hayo yanakwenda kitehema na hakuna gharama yoyote" amesema Makinda.

 Makinda anawahimiza watumishi wa umma wazungumzie kufanikisha Sensa ya mwaka huu, na Maafisa Habari ndiyo wataalamu wa habari, watumie nafasi yao kusaidia kuhamasisha wananchi kupitia mitandao ya kijamii kutoa elimu hiyo kwa kuwa wanaosoma zaidi mitandao ni vijana.

 Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi akiwa mkoani Tanga kwenye kikao kazi cha maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini Mei 12, 2022 amewahimiza wananchi kujitokeze kuhesabiwa siku hiyo ili kufikia malengo ya nchi.

"Maafisa Habari mnatakiwa kuelimisha wananchi umuhimu wa taarifa za majengo, na ni kwanini sensa ifanyike wakati huu. Ni vyema mkashiriki katika zoezi hilo kwa kutoa elimu sambamba na kubainisha changamoto na kutoa mrejesho hata kabla ya kuanza kwa sensa ya makazi" anasema Dkt Kijazi.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.