MTANGAZAJI

WATAFITI MUCE WAGUNDUA DAWA YA KUZUIA SUMU KUVU

Mtafiti Princess Ngowi kushoto akitoa maelezo kwa mkurugenzi wa NIMR Profesa Yunus Mgaya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho ya sita ya utafiti katika Chuo Kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa “MUCE

Watafiti kutoka Chuo Kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa “MUCE” cha mjini Iringa wamegundua dawa ya kuzuia sumu kuvu kwenye mazao ya nafaka inayotokana na mitishamba ugunduzi unaotajwa kuleta suluhisho katika uhifadhi wa mazao hayo

Akizungungumza katika maonesho ya sita ya utafiti Dkt. Juma Mongoyo ambaye ni Mkuu wa idara wa Kemia katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa amesema walifanya utafiti kupitia mmea aina ya Diospyros Mafiensis ambao uligunduliwa Mafia ambapo walitumia mizizi yake katika utafiti na kuleta matokeo chanya ya utafiti huo

Mongoyo alisema kuwa katika tafiti za mmea huo wamebaini kuwa mizizi yake hufanya kazi  ya kupunguza uzalishaji wa sumu kuvu na kulinda nafaka isishambuliwe na fangasi aina ya Asperigillus flavus na Asperigillus parasiticus wanaozalisha sumu kuvu kutokana na joto kali na unyevunyevu unaotengeneza fangasi hao.

 Dkt. Mongoyo alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa takribani watu milioni 4.5 duniani wanakula sumu kuvu kwa kiwango tofautitofauti ambapo huchukua miaka 30 hadi kujitokeza madhara yake huku akisema kuwa takwimu huonyesha takribani watu laki moja na elfu hamsini na tano hupoteza Maisha kila mwaka duniani kote  kutokana na tatizo la saratani ya maini inayosababishwa na ulaji wa sumu kuvu.

Alisema kuwa mizizi ya mmea huo wa diospyros mafiensis unauwezo wa kulinda nafaka na jamii yote inayoweza kushambuliwa na fangasi hao wajulikanao kama Asperigillus flavus na Asperigillus parasiticus

 Akizungumza mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye ni mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti wa magonjjwa ya binadamu “NIMR” Prof.Yunus Mgaya alisema kuwa taasisi ya NIMR imeona ipo haja ya kushirikiana na chuo cha Mkwawa  kutokana na tafiti hizo wanazozifanya zina lengo moja na taasisi ya NIMR ya kulinda afya ya binadamu 

Alisema kuwa tafiti iliyofanyika na Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es salaam Mkwawa kuhusiana na mmea unaotumika katika tiba asili ambayo wakatengeneza dawa yenye kemikali inayozuia  fangasi isizalishe sumu ambayo ikiingia kwenye mahindi yanayotumiwa na binadamu husababisha saratani ya ini hivyo utafiti huo unaweza ukakinga jamii dhidi ya magonjwa yatokanayo na sumu kuvu.

Maonesho hayo ya utafiti yanajumusha wanafunzi na waalimu watafiti kutoka Chuo Kikuu hicho kishiriki cha elimu ikiwa ni maandalizi ya kwenda kushiriki maonesho ya wiki ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yanayobeba kauli mbiu isemayo “utafiti na uvumbuzi endelevu kwa maendeleo ya viwanda”

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.