MTANGAZAJI

WAZIRI ATAKA MATUMIZI YA KISWAHILI KWENYE BIDHAA


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Abdallah Ulega amewataka wazalishaji wa bidhaa za ndani kuandika kwa Kiswahili maelekezo ya matumizi ya bidhaa wanazozalisha ili Watanzania waweze kuzisoma na kuzielewa.
 
Akizungumza katika ziara yake aaliyoifanya hivi karibuni katika ofisi za
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA),Ulega amewataka wazalishaji
mbalimbali wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania kutumia Kiswahili katika
maelezo yao ili bidhaa zipate kueleweka kwa watumiaji.


“Wazalishaji wote wa ndani na wa nje wanaoingiza bidhaa zao nchini waangalie
namna bora ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye bidhaa zao ambazo nyingi
zinaandikwa kwa lugha ya kigeni ili kuwawezesha Watanzania kuelewa maelekezo husika yaliyoko kwenye bidhaa hizo” alisema Naibu Waziri Ulega.
 
Ulega ameitaka BAKITA kusimamia ipasavyo zoezi hilo ili kuhakikisha Watanzania wanatumia bidhaa wanazozijua tofauti na sasa ambapo bidhaa nyingi zimeandikwa kwa lugha tofauti na Kiswahili.
 
 Naibu Waziri Ulega ametoa mwezi mmoja kwa BAKITA kusimamia na
kudhibiti  mfumo wa mapato yatokanayo na ithibati ya lugha ya Kiswahili ili
kuongeza mapato ambayo yamekuwa yakipotea kila siku kutokana na kuwepo kwa watafsiri wengi wa lugha ya Kiswahili wasiokuwa na ithibati.
 
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Bungeni Februari 11, 2021,kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki la kuitaka Wizara hiyo kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili kwa wageni wanaoingia nchini, Naibu Waziri Ulega ameitaka BAKITA kushirikiana na Wizara hiyo kuangalia namna ya kuanzisha madarasa hayo mapema iwezekanavyo.


“Hivi karibuni Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili kwa
wageni, nawataka BAKITA mshirikiane nao kuhakikisha madarasa hayo
yanaanzishwa”, alisisitiza Naibu Waziri Ulega.
 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.