MTANGAZAJI

MRADI WA KIDIJITALI KWA JAMII ZA PEMBEZONI

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania imefanya majadiliano na wawakilishi wa makundi mbalimbali kutoka katika jamii za pembezoni ambao ni wawindaji,wafugaji, wakusanya matunda na warina asali wa asili ili kujadili namna bora ya kutekeleza Mradi wa Tanzania ya kidijitali kwa kuepuka athari za kimazingira katika jamii hizo zinazotegemea mazingira katika kuendesha maisha yao ya kila siku.


Majadiliano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam, kwenye kikao baina ya Wizara hiyo, wawakilishi wa makundi hayo na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa Wizara ipo katika maandalizi ya kutekeleza Mradi wa Tanzania ya Kidijitali utakaoanza rasmi mwezi Julai mwaka huu na moja ya vitu muhimu inavyoangalia ni kuhakikisha mradi huo unakuwa jumuishi ili usilete athari kwenye mazingira na jamii kwa ujumla.


Aliongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo ni mpango wa Serikali kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano ya simu popote nchini na
kuongeza idadi ya matumizi ya intaneti kutoka asilimia 46 ya sasa hadi kufikia
asilimia 80 mwaka 2025 ili wananchi waweze kushiriki katika uchumi wa kidijitali kwa kutumia fursa nyingi zinazopatikana kupitia matumizi ya intaneti.


“Kuna maeneo wananchi wanaweza kupiga simu tu bila kupata huduma nyingine
zinazotumia intaneti kutokana uwepo wa minara yenye teknolojia ya 2G isiyoakisi mahitaji yaliyopo katika maeneo hayo. Mradi huu unaenda kuboresha matumizi ya teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili wananchi waweze kupata huduma nyingine za ziada”, Munaku.


Naye Rogasian Lukoa kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali
utazingatia haki na utu wa jamii za pembezoni na zinazotegemea mazingira katika kuishi kwa kubainisha mila na desturi zao na kuboresha jamii hizo ili ziweze kuendelea.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.