MTANGAZAJI

MAONESHO YA UTALII TANZANIA KUFANYIKA OKTOBA, 2021.

 

 

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inatarajia kufanya maonesho ya Kimataifa ya Utalii ( Swahili International Tourism Expo ) maarufu kama “SITE” yatakayoanza Oktoba 8 hadi 10, 2021 Mlimani City Jijini Dar es Salaam na kushirikisha Mawakala wa Utalii wa Kimataifa,waandishi wa habari za utalii wa Kimataifa, na wafanyabiashara wa utalii kutoka Tanzania na nchi za jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi, amesema Bodi kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania ng’ambo imejipanga kuwavutia mawakala wa utalii na waandishi wa habari za utalii wa Kimataifa kutoka nchi zao za uwakilishi pia kuvutia makampuni ya uoneshaji yapatayo 200 kutoka Tanzania, Nchi za Afrika Mashariki, Kati, Kusini na Afrika Magharibi.

“Kama kawaida yetu, onesho litakuwa na programu kadhaa zitakazo ongeza mvuto kwa mawakala wa kimataifa wa utalii, lakini pia tumejipanga kuendesha programu ya ziara ya mafunzo kwa baadhi ya mawakala wa utalii na waandishi wa habari za utalii wa Kimataifa ,
onesho litakuwa na programu za semina mbalimbali ambazo pamoja na masuala mengine zitalenga kutoa elimu kwa washiriki kuhusu mikakati ya kuvutia watalii katika kipindi hiki cha Janga la Corona, amesema Mdachi.

Aliongeza kuwa, SITE ya mwaka huu inabeba umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa mawakala wote wa utalii wa Tanzania kwa kuzingatia kuwa fursa za maonesho ya Kimataifa kama hayo bado hazijafunguka katika nchi nyingine kwa sababu ya changamoto ya ugonjwa wa
Corona.

Amebainisha kuwa, TTB ina uhakika wa kuwapata mawakala wa kimataifa, kutokana na makundi ya mawakala na watalii ambao imekuwa ikiwaleta baada ya Tanzania kufungua anga ambapo mpaka sasa Tanzania imeweza kupokea mawakala na watalii kutoka Nchi mbalimbali kama Urusi, Ukraine, Poland, Czech, Japani, Uhispania, Ufaransa, Uturuki na Uingereza .

Aidha, Mdachi ametoa wito kwa wadhamini, wadau, na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kutembelea onesho hilo ikiwa ni sehemu ya utalii wa ndani na kupata elimu kuhusu biashara za utalii lakini pia makampuni ya biashara za hoteli na mawakala wa utalii kuweza kutumia fursa zinazopatikana katika onesho hilo kwa ajili ya kujitambulisha na kujitangaza zaidi katika sekta ya utalii.

“Makampuni yenye uwezo wa kudhamini onyesho hili napenda kuwahakikishia kuwa udhamini wao kwa onesho la SITE ni fursa ya kipekee kujitambulisha kwenye sekta ya utalii ambayo inamatumaini makubwa kushamiri kwa kasi (To bounce back) mara dunia itakapofunguka.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.