FIONA AKOTH MWANADADA TOKA KENYA RUBANI WA NDEGE ZA JESHI LA MAREKANI
Miongoni mwa Habari iliyoandikwa na kujadiliwa na raia na watu mbalimbali toka Afrika Mashariki kwenye mitandao ya kijamii juma hili hasa mtandao wa twitter ni ya Msichana Fiona Akoth ambaye anakuwa Kijana wa Kike wa Kwanza kuwa Rubani wa Ndege za Jeshi la Anga la Marekani toka Kenya.
Fiona Akoth,anayetokea katika mji wa wavuvi pembezoni mwa Ziwa Victoria huko Kisumu,Kenya akiwa binti mdogo alilelewa na Babu yake na Bibi yake kwa kuwa Mama yake alihamia Marekani kwa masomo ambapo Fiona aliihamia Marekani akiwa na miaka 13 na kuanza masomo ya Sekondari katika jimbo la Texas.
"Nimekulia katika mazingira ya Kenya,ilinipasa kuacha familia,marafiki na ndugu nikiwa kijana mdogo na kwenda katika mazingira tofauti hii haikuwa jambo rahisi"anaeleza Akoth katika makala yake iliyoandikwa na mtandao wa Kituo cha Jeshi la Anga cha Columbus.
Fiona anasema baada ya kumaliza masomo ya Sekondari akaanza kutafuta vyuo,na ilibidi atafute ufadhili wa gharama za masomo kwa kuwa alijua wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kulipa gharama hizo na akafanikiwa kujiunga na Air Force Academy ambacho ndicho kilikuwa chaguo lake la kwanza japo wazazi wake walikuwa na wasiwasi wa yeye kujiunga na masomo hayo.
Anaeleza kuwa karibu na nyumbani kwao Kenya kulikuwa na Uwanja wa Ndege ambapo yeye na rafiki zake walikuwa wakifurahishwa kuona Ndege zikiruka na kutua na hapo ndipo alipogundua ndoto yake ya kuwa rubani.
Akoth anayezungumza Kiingereza na Kiswahili alihitimu Air Force Academy na kufanikiwa kujiunga kwa masomo zaidi na Kituo cha Jeshi la Anga cha Columbus kilichopo Mississippi.
"Imekuwa ni lengo langu kuwa rubani na Babu yangu mara zote aliniambia usikate tamaa katika kutimiza malengo yako na sasa niko hapa" anasema Fiona
Fiona anaeleza anatamani kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wa kike wa nyumbani anakotoka na yeyote aliye na njozi,Anapaswa kufanya kazi ya ziada na kujitoa zaidi na sasa anaishi katika njozi yake.
Post a Comment