MCHUNGAJI WA WAADVENTISTA WA SABATO NA BINTIYE WATEKWA HUKO HAITI
Waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani wamendelea kuomba kwa ajili ya kupatikana kwa Kiongozi wa Kanisa hilo katika Divisheni ya Inter-America Dkt Elie Henry na binti yake waliotekwa huko Haiti Disemba 24,mwaka huu huku mamlaka za nchini hiyo vikifanya jitihada za kupatikana kwao.
Taarifa za kuombea kupatikana kwa Mchungaji Henry na binti yake Irma Henry ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mazoezi ya Viungo kwa Wagonjwa katika hospitali iliyoko katika Mji Mkuu wa Haiti ,Port au Prince zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ya waumini wa Kanisa hilo Duniani Disemba 25 baada ya kuonekana kuandikwa kwenye Tovuti ya Hatiabones.
Tovuti hiyo ilieleza kuwa Mchungaji huyo aliondoka hospitalini hapo saa 12 jioni kwa gari binafsi kuelekea kwa ndugu yao katika eneo liitwalo Felmathe na mpaka hapo hawakuonekana ambapo Disemba 25 asubuhi watekaji walimpigia simu Kaka wa Dkt Henry wakidai kupatiwa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 5.
Akizungumza kwenye maombi maalum ya Watanzania Waadventista waishio Marekani Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani Mch Geoffrey Mbwana amesema Kanisa limepata taarifa hiyo na wanaendelea kuliombea ili Mchungaji huyo raia wa Haiti aliyekuwa likizo ya mwisho wa mwaka na Mkewe apatikane na kuungana na familia yake.
Henry ni Mchungaji wa Kanisa la Waadventista kwa miaka 40 sasa ambapo alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Divisheni ya Inter-America mwaka 2018.ambayo inajumuisha nchi ya Mexico,Karibiani ,Eneo la Kati mwa Bara la Amerika na sehemu ya Kusini mwa Bara hilo.
Post a Comment