TANZANIA YASHIKA NAFASI YA PILI KIDUNIA NA YA KWANZA AFRIKA MASHINDANO YA TEHAMA
Tanzania imeshika nafasi ya pili kidunia na ya kwanza katika bara la Afrika katika mashindano ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa mwaka 2020 yanayoratibiwa na Kampuni ya Huawei Tanzania katika vituo 14 vilivyopo kwenye vyuo vikuu nchini Tanzania.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizungumza kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa kutoa tuzo kwa washindi wa mashindano ya TEHAMA ambapo Tanzania imeshika nafasi ya pili kidunia na ya kwanza katika bara la Afrika Dkt. Ndugulile amesema kuwa ushindi huu unaakisi kuundwa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutambua mchango wa TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi; na kuchangia pato la taifa katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na uchumi wa kidijitali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imedhamiria kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye maeneo mengi zaidi nchini humo kwa lengo la kuongeza matumizi ya mawasiliano ya kasi ya brodibandi kutoka asilimia 45 ya sasa hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
Amesema Tanzania itatoa kipaumbele katika masuala ya utafiti na ubunifu sanjari na kuwatambua na kuwasajili wataalamu wa TEHAMA nchini ili kuwa na wataalamu wa kutosha kwenda sambamba na ukuaji na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Pia, amezitaka kampuni za ndani zinazojishughulisha na masuala ya TEHAMA ziige mfano wa kampuni ya HUAWEI kwa kuwekeza zaidi kwa kundi la vijana kwa nia ya kuibua na kuendeleza vipaji ambapo ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri TEHAMA katika shughuli za uzalishaji mali na na utoaji huduma katika sekta mbali mbali ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo HUAWEI kuhakikisha kuwa inaendelea kuanzisha vituo vya umahiri vya sayansi na teknolojia kwenye taasisi za elimu ya juu nchini kwa kuzingatia maeneo ya kimkakati katika kujenga uchumi imara.
Post a Comment