VIONGOZI DINI NA SERIKALI TANZANIA WAMLILIA MUNGU DHIDI YA CORONA (+VIDEO)
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini
nchini Tanzania wameendesha maombi maalum ya kuiombea nchi hiyo dhidi ya maambukizi ya virusi vya
Corona.
Maombi hayo yamefanyika katika Viwanja vya
Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim
Majaliwa.
Akizungumza kabla kuanza rasmi kwa maombi hayo,
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hadi Aprili 21,2020, Watanzania 284
walithibitika kuambukizwa Corona, 256 wanaendelea vizuri, saba wako chini ya uangalizi,
11 wamepona na kurejea makwao na watu 10
wamefariki Dunia.
Amesema kuwa Serikali inatambua jitihada kubwa
inayofanywa na viongozi wa Dini katika kuhamasisha waumini wao kuzingatia
masharti na tahadhari dhidi ya Corona.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa ni lazima kuzingatia
maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya kwani yatasaidia kuondokana na
maambukizi nchini na kupunguza uwezekano wa kuwa na maambukizi mapya ambapo amewataka wazazi na walezi nchini kudhibiti
mizunguko isiyo lazima kwa watoto wao ili kukabiliana na maambukizi mapya.
Aidha amezitaka kamati za ulinzi na usalama za
mikoa kuzingatia masharti ya kinga dhidi ya ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia
ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa ikiwemo Sukari hasa
kipindi hiki kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Wakiongoza maombi hayo ya kitaifa baadhi ya viongozi
wa dini wamemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli kwa kuruhusu kuabudu na kuliombea taifa dhidi ya janga la Corona
nchini.
Kwa upande wake Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari
Zubeir alimwomba yarabi kuondosha mtihani huo wa Coronaamabao umeitikisa dunia
kwasasa na kuomba waumini kuendelea kuomba kwajili ya kuondokana na janga hilo.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Jude
Thadeus Rwaichi amesema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wa Maisha ya mwandamu
hivyo ni budi kumuomba yeye ili atupitishe salama na kuondokana na janga hili
la Corona.
Viongozi wa Dini walioshiriki maombi hayo ni kutoka Madhehebu ya Roman Katoliki,Kiislamu, Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Jumuiya
ya Mabohora, Kanisa la Pentekoste, Kanisa la Waadventista wa Sabato, Mwakilishi wa Mufti wa
Zanzibar na wafuasi wa madhebu ya Budha Tanzania.
Maombi haya dhidi ya maambukizi ya homa kali ya
mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona ni mwendelezo wa maombi ya kitaifa
yaliyoitishwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia Aprili 17 hadi 19, 2020 kote nchini Tanzania.
Mapema Aprili 9, 2020 Viongozi wa Dini na
baadhi ya Viongozi wa Serikali walikutana jijini na Dar es Salaam na kuazimia
kufanyika kwa maombi maalum ya kitaifa yanayoshirikisha waumini wa madhebu yote
nchini Tanzania ili kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Post a Comment