MAKANISA YA WAADVENTISTA TEXAS MAREKANI RUHUSA KUFANYA IBADA KWA MASHARTI
Mwenyekiti wa Konferensi ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ya Texas nchini Marekani Carlos Craig (katikati) akizungumza na waumini wa Kanisa hilo kupitia mtandao wa Kijamii wa Facebook |
Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Konferensi ya Texas nchini Marekani umetangaza rasmi ruhusa ya makanisa katika eneo hilo kuendelea na ibada za siku za Sabato baada ya tangazo la Serikali ya Jimbo la Texas lililotolewa Aprili 27,2020 kupitia kwa Gavana Greg Abbot kutangaza kwa wakazi wa jimbo hilo kuendelea na shughuli kama kawaida baada ya kuwekwa karantini kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na janga la Corona.
Akizungumza jana Aprili 27 kwa njia ya Mtandao wa Kijamii wa Facebook kupitia Facebook live Mwenyekiti wa Konferensi ya Texas Carlos Craig amesema makanisa yanapaswa kuanza huduma za ibada kuanzia Mei 3 mwaka huu lakini yakizingatia taratibu na kanuni za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona yanayotolewa na wataalamu wa Afya ikiwemo kuzingatia umbali wa hatua sita toka mtu mmoja na mwingine,kuvaa Barakoa huku akisitiza kuwa taratibu na miongozi mingine zitatumwa kwa makanisa jumahili na kuandikwa katika tovuti ya konferensi hiyo.
Toka kuwekwa kwa agizo la Karantini nchini Marekani mwezi Machi mwaka huu kutokana na kujikinga na janga la Corona waumi wa makanisa mbalimbali wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii katika kufikisha maudhui ya ibada kwa waumini wao wakiwa nyumbani.
Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni kupitia tovuti yake ya takwimu inaonesha kuwa Konferensi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1907 hadi mwishoni mwa mwaka 2018 ilikuwa na idadi ya makanisa 250 yakiwa na idadi ya waumini 60,591.
Tovuti ya Konferensi ya Texas imeeleza kuwa kama kutaonekana visa vya Covid-19 katika makanisa ya Konferensi hiyo,makanisa husika yatarejea katika hali ya kufungwa tena kama ilivyokuwa mwezi Machi 2020.
Tovuti hiyo pia imeeleza kuwa ruhusa hiyo ya kuyafungua makanisa kwa ajili ya ibada itazingatia awamu tatu ya mwongozo ambapo awamu ya kwanza inayataka makanisa kufanya huduma ya mahubiri bila huduma zingine,kuzingatia usafi wa kuwepo kwa vitakasa mikono,kuzingatia umbali wa mshiriki na mshiriki akiwa kanisani na kuhusisha watu wachache kwa muda wa majuma manane huku huduma za ibada ya mtandaoni zikiendelea.
Awamu ya pili itaanza baada ya majuma manne kwa makanisa kuendesha mahubiri kama kutakuwa hakuna kesi mpya za maambuzi ya Covid-19 na kufuata miongozi inayotolewa na wataalamu wa Afya wa eneo husika huku makanisa hayo yakizingatia kufanya usafi wa kujilinda na virusi vya Corona kabla na baada ya kumaliza mikusanyiko ya ibada.
Awamu ya tatu imeeleza kuwa makanisa yataendelea na taratibu za ibada kama ilivyokuwa kabla ya kuwekwa karantini iwapo hakutakuwa na matokeo hasi ya awamu ya kwanza na ya pili.
Post a Comment