MTANGAZAJI

KONFERENSI YA KANISA LA WAADVENTISTA MAREKANI YATANGAZA KUPUNGUZA WAFANYANYAKAZI







Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Konferensi ya Texas nchini Marekani umetangaza  kuwaondoa kazini wafanyakazi wake 32 ili kupunguza matumizi ya fedha katika Konferensi hiyo ambayo inakabiliwa na upungufu wa fedha uliosababishwa na ufinyu wa bajeti na kushuka kwa matoleo kutoka kwa waumini wake ambao pia umechangiwa na ukosefu wa ajira miongoni mwao kutokana na janga la Corona.

Idadi hiyo ni miongoni mwa wafanyakazi  500 wa Konferensi hiyo ambao hawakuwa wamechukua fedha za kujikimu wakati wa Karatini kutokana na janga la Corona  zilizotolewa na serikali ya Marekani kwa wakazi wa nchi hiyo  hivi karibuni.

Taarifa hiyo imetolewa kupitia mkutano wa Viongozi wanne  wa juu wa  Konferensi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Konferensi hiyo  Carlos  Craig na kurushwa mbashara kupitia mtandao wa Facebook ukishuhudiwa na watu 371 ambao walishiriki kwa kutazama na kuuliza maswali mkutano huo ulioendeshwa kwa lugha ya Kiingereza na Kihispaniola kwa muda wa saa mbili na dakika 14.

Uongozi huo umeeleza kuwa mkakati wa kukabiliana na upungufu wa fedha za uendeshaji utaanza Mei Mosi mwaka huu hadi Julai Mosi mwaka huu ambapo  wafanyakazi waotarajiwa kuondolewa kazini ni 6 waliokuwa wakifanyakazi kwa masaa maalum  katika Konferensi,Wachungaji 11,na walimu wa Biblia 15, pia kuondoa gharama za safari kwa wachungaji,Wakuu wa shule na walimu wa Biblia,huku akieleza kuwa wametoa mwanya wa kujiondoa kwa hiari kwa watumishi walio na miaka zaidi ya 65 na kuendelea na wastafu waliokuwa  wakifanya kazi kwa mikataba nje ya mafao yao .

Mkakati mwingine uliowekwa ni kupunguza saa za kazi kutoka 40 kwa juma hadi saa 20 kwa juma kwa watumishi katika  ofisi za  Konferensi hiyo.

Kutona na ukosefu wa fedha za kulipa wachungaji Mwenyekiti huyo wa Konferensi ya Texas iliyoanzishwa mwaka 1907 amesema viongozi wa juu na wakurugenzi wa Idara wataanza kusimamia baadhi ya makanisa ambayo yatakosa wachungaji baada ya zoezi la kuwaondoa kazini wachungaji.

Alipoulizwa kuhusu matumizi ya fedha  za uendeshaji wa  konferensi hiyo  kwa mujibu wa bajeti ambayo inategemea zaka za  matoleo ya waumini Mhazini wa Konferensi ya Texas Randy Terry amesema kuwa bajeti ya uendeshaji ni dola milioni 52 kwa mwaka huku alieleza kuwa mpaka mwezi Februari mwaka huu  walikuwa wametumia dola milioni 5 kwa mwezi   ambapo  jumla ya makanisa 200 yameshindwa kutoa zaka kwa njia ya mtandao hasa katika kipindi cha Karantini.


Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni kupitia tovuti yake ya takwimu inaonesha  kuwa Konferensi hiyo hadi mwishoni mwa mwaka 2018 ilikuwa na idadi ya makanisa 250 yakiwa na idadi ya waumini 60,591,huku idadi ya wachugaji hadi mwaka 2014 ikiwa ni 130 waliowekewa mikono na wenye leseni pekee yake wakiwa ni 24.

Tovuti ya Konferensi hiyo ambayo imetoa baadhi ya  majibu ya maswali yaliyoulizwa kwenye mkutano huo imeeleza kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji cha Konferensi ya Texas kilichoketi kabla ya Janga la Corona kilipitisha maamuzi ya kukabiliana na ukata wa bajeti kwa kuamua kuwa kutopitisha pendekezo la kuongeza asilimia 1.6 kwa wafanyakazi,kupunguza asilimia 25 ya bajeti za idara,kutofadhili mikutano ya makambi kwa mwaka 2020,kusitisha gharama za matibabu kwa mwaka 2021 kwa wanandoa ambao wenzi wao wanabima za matibabu na kupunguza Dola za Kimarekani 150,000 kutoka katika  bajeti ya mwaka 2020.




No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.