BREATH OF LIFE TV KUSAIDIA UJENZI WA KANISA CHATO TANZANIA.
Mkurugenzi wa Global Vessels Organization ya nchini Marekani Fraiser Martis akihojiwa na Hope Channel Tanzania akiwa katika uwanja ambapo panatarajiwa kujengwa Kanisa mjini Chato Tanzania |
Kituo cha Televisheni cha Breath of Life cha Marekani kwa kushirikiana na Global Vessels Organization iliyoko Alabama nchini humo watasaidia ujenzi wa Kanisa la Waadvetista wa Sabato jipya mjini Chato nchini Tanzania baada ya kushuhudia idadi kubwa ya watu waliobatizwa kwenye mkutano wa Chato 2020 MUNGU KWANZA uliofanyika mjini humo ambapo Dkt Carlton Byrd ambaye ni Mkurugenzi wa Breath of Life alihutubu kwa majuma mawili.
Hadi kufikia Machi 8 mwaka huu idadi ya watu waliobatizwa nchini Tanzania kutokana na mkutano wa Chato 2020 MUNGU kwanza uliodumu kwa majuma matatu yaliyomalizika Machi 7 mwaka huu ni 13,920 huku takwimu zikionekana kuongezeka ambapo zaidi ya watu 600 wanatoka mjini Chato.
Taarifa ya Machi 6 mwaka huu ya chapisho la mtandaoni la kila juma la Kituo cha Televisheni cha Breath of Life imeeleza kuwa Kanisa hilo litaitwa Breath Of Life Chato na litajengwa kwa ushirikiano na Kanisa la Chato ambalo limeshatoa kiwanja kwa kushirikiana na Uongozi wa Kanisa hilo nchini Tanzania.
Chato ni moja ya wilaya tano za mkoa wa Geita ulioko Kaskazini Magharibi mwa Tanzania,makao makuu ya Wilaya ya Chato ni Chato Mjini nyumbani kwao na Rais wa awamu ya Tano nchini Tanzania John Pombe Magufuli ambaye alizaliwa Chato Oktoba 29,1959.
Chato mjini kuna makanisa ya Waadventista wa Sabato matatu huku kanis litakalojengwa likitarajiwa kuongeza idadi ya makanisa mjini humo na kuwahudumia miongini mwa waumini waliobatizwa kutokana na Mkutano wa Chato 2020 MUNGU KWANZA.
Mkutano wa Chato 2020 MUNGU KWANZA uliokuwa ukirushwa mbashara na Vyombo vya Habari vya Kanisa la Waadventista Tanzania (Morning Star Radio,Hope Channel Tanzania,Rock FM) na kudhaminiwa na Chama cha Wajasiriamali na Wanataaluma nchini Tanzania (ATAPE) na Umoja wa Watanzania Waadventista waishio Marekani (TAUS) ulihitimishwa Machi 7 mwaka huu.
Post a Comment