MTANGAZAJI

WAADVENTISTA TANZANIA WAZINDUA CHATO 2020 MUNGU KWANZA

(Picha zote kwa hisani ya NTUC Media)
Katibu Mkuu wa Union ya Kusini  mwa Tanzania katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Dkt. Rabson Nkoko amezindua rasmi maandalizi ya kuelekea kufanyika  Mkutano wa Injili wa Mungu Kwanza utakaofanyika mjini Chato,Geita Tanzania Februari  15 hadi Machi 7 mwaka 2020.

  Uzinduzi huo ambao pia ulihudhuriwa na Viongozi wa Kitaifa wa Umoja wa Wajasiriamali na Wanataaluma Waadventista nchini Tanzania (ATAPE) ambao ndio wadhamini wa Mkutano huo utakaorushwa na Vyombo vya Habari vya Kanisa hilo Morning Star Radio,Rock FM na Hope Channel Tanzania ulihudhuriwa na zaidi ya watu 5000 kutoka viunga mbalimbali vya Mji wa Chato na mikoa jirani, huku kwaya 62  kutoka makanisa  mbalimbali ya Jimbo la Magharibi mwa Tanzania(WTC) lenye makao yake makuu mkoani  Kigoma zikishiriki kutoa huduma ya uimbaji.

Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Charles Kabeho ambaye alihudhuria uzinduzi huo uliofanyika katika Viwanja vya Kanisa la Waadventista wa Sabato la Chato Mission amelihakikishia Kanisa la Waadventista wa Sabato kuwa atashirikiana nalo bega kwa bega kuhakikisha Mkutano huo unafanikiwa.

Akizindua mkutano huo Mchungaji Nkoko amesema kuwa mkutano huo utakuwa wa aina yake kutokana na aina ya wahudumu watakaokuwepo pia unafanyika nyumbani kwao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli. 

Mwenyekiti wa  ATAPE, Freddie Manento amesema kuwa mkutano huo utaambatana na kuwepo kwa  kambi za Afya zaidi ya Tano kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita ikiwemo Chato ambako  kitakuwa Kituo Kikuu cha Mkutano.

  Wahutubu kwenye Mkutano huo wenye Kauli Mbiu ya MUNGU kwanza ni  Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha  Breath of Life na Mchungaji wa Kanisa la Chuo Kikuu cha Oakwood cha nchini Marekani  Dkt Carlton P.Byrd akisaidiana na Dkt Godwin Lekundayo ambaye ni Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Union Konferensi ya  Kaskazini mwa Tanzania.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.