MIUNDOMBINU YA KITUO CHA FORODHA CHA HOROHORO HAIKIDHI VIWANGO-SERIKALI
Serikali ya Tanzania imetoa agizo kwa
watendaji wa Kituo cha pamoja cha Forodha Mpakani- Horohoro, kuwasilisha
nyaraka za ujenzi wa Kituo hicho ukiwemo mkataba, kwa kuwa miundombinu iliyopo
haijakidhi viwango jambo lililosababisha kutofunguliwa rasmi kwa kituo hicho
tangu mwaka 2015.
Agizo hilo limetolewa na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro walipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Kituo
hicho ambapo hawakuridhishwa na miundombinu yake.
Dkt. Kijaji, alisema kuwa
Kituo hicho hakina mawasiliano kati ya upande wa Tanzania na Kenya hivyo
kutokidhi vigezo vya kuwa Kituo cha pamoja cha Forodha kati ya nchi hizo mbili.
Alisema kuwa ukosefu wa
mawasiliano unasababisha urasimu katika kuwahudumia wananchi jambo linalosababisha
wateja katika mpaka huo kutafuta njia nyingine ambazo sio rasmi katika
usafirishaji bidhaa jambo ambalo linaathari kubwa katika ukusanyaji wa mapato.
Miongoni mwa kasoro
zilizobainika wazi ni kamera maalum za usalama zinazotakiwa kufanyakazi ni
zaidi ya 14 lakini zinazofanyakazi mpaka sasa ni 4 pekee jambo linalotiashaka
kuhusu usalama wa Kituo hicho
Dkt. Kijaji, alisema pia,
utaratibu wa wakazi wa Horohoro kwenda kupata huduma za TRA katika Wilayani
Muheza usitishwe na badala yake watumishi wa Mamlaka hiyo waende kuwahudumia
wananchi katika Wilaya ya Mkinga ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara
wanapotaka kulipa kodi au kutafuta huduma za masuala ya forodha.
Aidha, Manaibu Waziri hao wameiagiza
Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Tanga kuhakikisha Jenereta la Kituo hicho cha
Pamoja cha Forodha linafanyakazi ndani ya saa 24 ili kukabiliana na upotevu wa
mapato katika eneo hilo kinyume na hapo hatua zingine zitachukuliwa.
Manaibu Waziri hao wametoa
maagizo hayo baada ya kuelezwa kuwa jenereta halifanyikazi baada ya kuharibika
kwa takribani siku 14 na kusababisha Seikali ikose mapato na kuleta usumbufu
kwa watumiaji wa Kituo hicho kwani hulazimika kukaa muda mrefu kusubiri umeme
urejee baada ya kukatika.
Post a Comment