MPAKA KATI YA TANZANIA NA KENYA KATIKA KIJIJI CHA MAHANDAKINI TANGA BADO NI CHANGAMOTO
Serikali ya Tanzania imeahidi kutatua
mgogoro wa Mpaka kati ya Tanzania na Kenya katika Kijiji cha Mahandakini,
Wilayani Mkinga mkoani Tanga, baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wanakijiji
wanaoishi katika mwambao huo wa Bahari ya Hindi baada ya kuzuiwa kufanya
shughuli zao za uvuvi na kuwasababishia hali ngumu ya maisha.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro walipotembelea
na kukagua eneo hilo la mpaka na nchi Jirani ya Kenya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mahandakini, Bw. Nasoro Mbarook, alisema
kuwa wavuvi wa Kijiji hicho wanashindwa kuendelea na shughuli za uvuvi baada ya
vifaa vyao vya uvuvi kukamatwa na wavuvi
takribani 112 kukamatwa na vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Kenya
nakufunguliwa mashtaka kisha kutozwa faini ya Sh. 5000 ya Kenya, jambo ambalo
wavuvi hao wanaamini halikua sahihi kwa kuwa walikua wanavua katika maji ya
Tanzania katika Bahari ya Hindi hivyo hawakutenda kosa kama ilivyodaiwa.
Manaibu Waziri hao, walisema
dhumuni la ziara yao katika mpaka huo ni kujionea hali halisi na pia kuweka
mikakati ya namna ya kutatua changamoto
zilizopo ikiwemo ya wananchi kushindwa kulipa kodi kutokana na kukosa kipato
kilichotokana na uvuvi ambapo kwa sasa wanazuiwa kufanya shughuli za uvuvi.
Walisema kuwa wamejionea
hali halisi ya mpaka huo hivyo Serikali itafanya tathmini kisha kufanya
majadiliano na wenzao wa Kenya ili kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Aidha walibaini kuwa eneo
la mpaka halijazingatia taratibu kwa
kuwa zipo nyumba ambazo zimejengwa chini ya umbali wa mita 30 mahali ambapo palipaswa kutokuwepo makazi
hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Mkinga Bw. Yona Mark, ameiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha
ujenzi wa Shule ya Msingi katika Kijiji cha Mandakini Wilayani humo ili
wanafunzi waanze kusoma kwa kuwa kwa sasa watoto wanasoma katika shule iliyopo
eneo la Kenya.
Post a Comment