MTANGAZAJI

DK. HAMISI KIGWANGALLA AMEAGIZA RASIMU YA SERA MPYA YA MISITU IKAMILIKE NDANI YA MWEZI HUU WA NOVEMBA

Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwasili katika ukumbi wa Hoteli ya Morena mjini Dodoma jana kwa ajili ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza kukamilishwa haraka kwa rasimu mpya ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 2016 ili kuwezesha upatikanaji wa Sera, Sheria na Kanuni mpya za usimamizi wa rasilimali za misitu nchini kwa ufanisi zaidi.

Ameagiza wataalamu wa Wizara hiyo kukamilisha rasimu hiyo mwezi huu wa Novemba na iwasilishwe kwake mapema mwezi ujao (Desemba) ili aweze kupata ushauri zaidi wa wataalamu wengine huru kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri na baadaye kutungiwa Sheria na Kanuni za utekelezaji.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo mjini Dodoma wakati akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa misitu iliyolenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.
Alisema amelazimika kuharakisha zoezi hilo ili Sera hiyo ikamilike haraka iweze kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo ongezeko la watu linalosababisha misitu mingi kuteketezwa kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kupitia shughuli za kilimo na uanzishwaji wa makazi mapya.

Alisema pamoja na misitu kuonekana inachangia kidogo kwa asilimia 3.5 kwenye pato la taifa, bado mchango wake ni mkubwa kuliko inavyochukuliwa hivi sasa. Alisema tafiti zilizofanywa awali hazikuzingatia mambo muhimu ikiwemo mchango halisi wa misitu kwenye upatikanaji wa maji ambayo huzalisha umeme, hunywesha mifugo na wanyamapori, matumizi ya majumbani na kilimo cha umwagiliaji.

Alisema ili kupata mchango halisi wa misitu kwenye uchumi mpana wa taifa letu, Wizara yake imeshaandaa andiko maalum kwa ajili ya kuendesha utafiti mkubwa wa kubaini mchango huo na kazi inayofanyika hivi sasa ni ya utafutaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kufanikisha utafiti huo.

Akizungumzia Uhifadhi Shirikishi Jamii, Dk. Kigwangalla alisema kwa zaidi ya asilimia 32 ya maeneo yote nchini yamehifadhiwa kisheria, hivyo njia rahisi ya kuyalinda ni kupitia ushirikishwaji wa wananchi. "Bila kufanya hivyo hatuwezi kusema tuna askari wa kutosha kulinda misitu yote, mbuga zote za wanyama au mapori yote tengefu nchini.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.