ASILIMIA 80 YA WAKAZI WA MWANZA HAWANA VYOO BORA
Wakati serikali ya Tanzania ikiwa imetiliana saini Mkataba na Benki ya Kitega uchumi ya Umoja wa
Ulaya(EIB)na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD)ili kutekeleza Mradi wa Maji
safi na Mazingira ya Jiji la Mwanza,utafiti unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Mwanza hawana
vyoo bora,na hutiririsha maji taka kikiwemo kinyesi katika ziwa
Victoria ambapo asilimia 85 ya wakazi wa jiji hilo hawajaunganisha maji taka yao katika
mfumo wa maji taka ulioko Butuja.
Mkataba huo
umesainiwa Machi 5 mwaka huu, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji ya
kunywa kwa wakazi wa Jiji la Mwanza,hususan katika maeneo ambayo hadi sasa
hulazimika kunywa maji ya visima,kwa kuwa hayafikiwi na maji ya bomba.
Mradi huo utawezesha usafi wa mazingira kwa wakazi wa milimani katika jiji hilo,ikiwa
ni pamoja na kujenga vyoo katika shule za msingi ambazo wanafunzi zaidi ya 100
hulazimika kutumia tundu moja la choo kwa siku.
Mkurugenzi
wa Maji Safi na Maji Taka jijini Mwanza,MWAUWASA,Mhandisi Anthony Sanga,
ameiambia amewaambia waandishi wa habari leo kwamba, mradi huo mkubwa wa matangi
makubwa,utaongeza maji kwa kiasi cha mita za ujazo 50,000 kwa siku.
Kulingana na
Mhandisi huyo wa MWAUWASA,Anthony Sanga,mradi huo ukikamilika utaondoa kero ya
maji kwa wakazi wa maeneo ya Buswelu,Kiseke,Ibanda,Kabuhoro,Kirumba na maeneo
mengine ya jiji ambako akina mama hulazimika kudamka usiku wa manane kutafuta
maji.
Kulingana na
MWAUWASA,Mradi huo wa usafi jijini Mwanza ni utekelezaji wa Matokeo Makubwa
sasa(BRN),na lengo ni kuondoa tatizo la maji salama na uchafuzi mkubwa wa
mazingira unaofanywa na wakazi wa milimani.
Na:Conges Mramba
Post a Comment