MTANGAZAJI

WAZIRI MKUU WA TANZANIA AMEONYA KUTOSHABIKIA MAAFA


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya watu wanaofanya ushabiki wa kisiasa kwenye tukio la mlipuko wa Arusha na kuwataka wasitumie tukio hilo kujipatia umaarufu na badala yake watumie fursa hiyo kuwafariji walioathirika na kuwa watulivu hadi suala hilo lifikie hatma yake.
Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni kubwa, na kitendo hicho ni kibaya kinachostahili kulaaniwa vikali kwa hiyo haifai watu wachahe kujipatia umaarufu kupitia tukio hilo.

Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Mei 7, 2013) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea ili kuwajulia hali majeruhi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha.

Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na hali ya utulivu wa wananchi wa Arusha na hasa waliokaribu na Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, kufuatia mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu.
Alisema ameguswa pia na hali ya matibabu inayotolewa kwa majeruhi katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha.
Waziri Mkuu alikatisha shughuli za Bunge juna mchana na kuelekea Arusha. Mara baada ya kuwasili KIA juna jioni, Waziri Mkuu alikwenda moja kwa moja Parokia ya Olasiti ili kujionea hali halisi na kuwapa pole wamunini wa Kanisa hilo.

Baadaye alikwenda kumjulia hali Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican, Mhashamu Askofu Fransisko Padilla ambako alifanya nao mazungumzo na kuwahakikishia viongozi hao kwamba Serikali itafanya kila iwezalo hadi iwabane wahusika.

Akiwa hospitali ya Mount Meru leo asubuhi, Waziri Mkuu alimweleza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti kuwa asisite kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Magesa Mulongo endapo hali ya majeruhi itabadilika na watahitaji matibabu zaidi.

Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikabidhi vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 23.3 ambavyo ni dawa na vifaa tiba kwa uongozi wa hospitali hiyo ambavyo vilitolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) chini ya uhamasishaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kukabidhi misaada hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema juzi (Jumatatu, Mei 6, 2013), TANAPA ilitoa mablanketi 50 hospitali hiyo na kwamba wafanyabiashara wa sekta ya utalii wa mjini Arusha wamejipanga kutoa msaada zaidi ili kuisaidia hospitali hiyo kumudu kuwahudumia majeruhi wa mlipuko huo.

Hadi sasa, watu watatu wamepoteza maisha kutokana na mlipuko huo ambapo watu wanane wamekamatwa na kuhojiwa na polisi. Kati yao, wanne ni raia wa Saudi Arabia na waliobakia ni wakazi wa Arusha. Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tulio hilo.

Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema wagonjwa watatu wana hali mbaya ambapo mgonjwa mmoja yuko Muhimbili na wawili wako hapo hapo Mount Meru.

“Watu 66 waliathirika na mlipuko huo, watatu wamefariki na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wagonjwa 24 wamesharuhusiwa kurudi nyumbani, waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu,” alisema.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma mchana huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P 980,
DODOMA.
JUMANNE, MEI 7, 2013.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.