TAARIFA YA TISHIO LA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO)
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
|
TAARIFA KWA UMMA
TAHADHARI
LA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO)
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii imepokea taarifa mnamo tarehe 22 Mei 2013 kutoka Shirika la
Afya Ulimwenguni, (WHO) ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kupooza (Polio) katika
Wilaya ya Fafi nchini Kenya. Mpaka sasa kuna mgonjwa mmoja bila kifo.
Ugonjwa wa
Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kama “Polio Virus”. Ugonjwa huu unaathiri
misuli na mfumo wa fahamu hivyo kusabisha kupooza kwa viungo hasa miguu na hata
kifo. Ulemavu huu ukishajitokeza huwa ni wa kudumu. Waathirika wakuu wa ugonjwa
huu ni watoto hasa walio na umri chini ya miaka mitano. Hata hivyo ugonjwa huu
unazuilika kwa chanjo ya Polio ambayo ni salama na inatolewa bure na Serikali
katika vituo vyote vya huduma ya afya. Mtoto aliyepata chanjo ya Polio anakuwa
amekingwa na ugonjwa wa Polio kwa maisha yake yote.
Kutokana
na taarifa hiyo ya kutoka nchini jirani ya Kenya, baadhi ya mikoa ina uwezekano
mkubwa wa kupata maambukizo ya ugonjwa huo kufuatia ushauri wa kitaalam. Aidha,
mikoa hii mingine inapakana na nchi jirani ya Kenya na mingine ina mapungufu
yaliyopo katika hali ya chanjo ya Polio. Mikoa hii ni pamoja na Dar es Salaam,
Pwani, Tanga, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara na Mwanza.
Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la
ugonjwa huu:
·
Kutoa taarifa ya
tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya.
·
Kuimarisha ufuatiliaji
wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya
mipaka
·
Kufuatilia kwa karibu
hali ya chanjo mikoani na wilayani hususan ya Polio hususani iliyo katika
hatari ya maambukizi
·
Kuhamasisha watoto ambao hawajakamlisha
ratiba yao ya chanjo hususani ya Polio au ambao hawajapata ya chanjo hii waweze
kwenda vituo vya karibu vya afya vya kutolea chanjo
Wizara
inapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa ngazi zote
kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kila mtoto mlengwa anapata chanjo ya Polio. Aidha
Wizara inatoa rai kwa wadau wetu, taasisi za dini, taasisi zinazofanya kazi
katika jamii na vyombo mbalimbali kuhamasisha watu wapeleke watoto wao kwenye
vituo vya huduma wakapewe chanjo hii muhimu. Chanjo hii ni salama na inatolewa
bila malipo.
Wananchi
wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara wanapoona
au kupata taarifa
ya mtoto yoyote anayepata ulemavu wa ghafla pasipo sababu yoyote. Mtoto huyo
apelekwe katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na hatua za haraka.
Imetolewa na;
Nsachris Mwamwaaja
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
30/05/2013
Post a Comment