MCT- MSANII LULU AHUKUMIWA NA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), imeeleza kusikitishwa kwake na ukiukwaji wa maadili uliojitokeza wakati wa kuripoti kesi ya mshtakiwa Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati, Jaji Thomas Mihayo, alisema kuwa, baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, kesho yake baadhi ya vyombo vya habari vilimhukumu kuwa ni muuaji kupitia vichwa vya habari vya magazeti.
Alisema kwa mujibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama.
Jaji Mihayo alisema kuwa, MCT imetoa matamko mara kadhaa kuwakumbusha wanahabari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.
Alisema baraza linafahamu kuwa kesi zilizopo mahakamani ni kivutio kwa umma kwa sababu hutaka kujua kinachoendelea ili haki itendeke. Pia wanahabari nao wanahaki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sheria.
“Ifahamike kuwa wakati wakitumia fursa na haki hiyo, wanapaswa kuzingatia kanuni, miongozo na sheria zinazolinda haki ya msingi ya mtuhumiwa na uhuru wa mahakama” alisema.
Alisema kuwa, vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti baada ya kesi huyo viliingilia uhuru wa mahakama kwa kuchapisha habari zinazoshawishi au kushinikiza uamuzi wa muhimili huo.
Aidha, alisema nchi nyingine duniani, mshtakiwa kama Lulu ni mtu muhimu sana na hulindwa kwa sababu ndiye anayejua ukweli wa tukio zima.
Aliwataka Wahariri wa vyombo vya habari kuacha kutafuta vichwa vinavyouzia magazeti yao ambavyo vimekuwa vikihukumu.
Pia aliwaasa wanahabari kuwa makini kwa sababu sio kila kitu wanachozungumza polisi kinatakiwa kuandikwa haswa kinachohitaji uchunguzi.
“Kisheria uchunguzi unatakiwa ufanyike kwa siri ndio maana kila kitu hupelekwa mahakamani, hata kama jalada la kesi limefikishwa kwa DPP, yeye anapaswa kukueleza kama amelipokea au la na si vinginevyo,” alisema.
Kuhusu baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo nayo iliripoti kuhusu kesi hiyo, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Kajubi Mukajanga, alisema ingawa katiba ya MCT haijajumuisha mitandao hiyo, lakini haikufurahishwa na jinsi ilivyotoa taarifa za msanii huyo.
Mukajanga alisema kuwa, tatizo lililopo ni baadhi ya watu wanaoendesha mitandao hiyo sio wenye taaluma ya habari.
“Kwa ujumla habari kama hizi za kutoa hukumu wakati kesi zikiendelea mahakamani sio mzuri hata kidogo, iwe kwa watu wenye taaluma hii au la,” alisema.
“Kwa ujumla habari kama hizi za kutoa hukumu wakati kesi zikiendelea mahakamani sio mzuri hata kidogo, iwe kwa watu wenye taaluma hii au la,” alisema.
Alipoulizwa kama baraza hilo limepokea malalamiko yoyote yanayolalamikia vichwa hivyo vya habari, Mukajanga alisema hadi jana hawajayapokea huku Jaji Mihayo kwa upande wake akisema kuwa, mtendaji bora wa kazi hapaswi kungojea malalamiko.
Mukajanga alisema hatua ambazo wamezichukua kama kamati ni kuwaandikia barua Wahariri wote wa vyombo vya habari kuwakumbusha wajibu wao katika kuripoti habari kama hizo.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rose Haji, alisema kuwa, wakati kesi hiyo iliripotiwa kwenye vyombo vya habari, alitegemea ingeandikwa kwa hisia chanya badala yake, habari zililenga kumkandamiza na kumdhalilisha mshtakiwa huyo.
Alisema katika tukio hilo, mambo ya udhalilishaji yaliongezeka licha ya hivi karibuni viongozi mbalimbali toka Bara la Afrika kufika hapa nchini kupanda mlima Kilimanjaro huku wakilenga kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya mwanamke.
Post a Comment