MTANGAZAJI

TUME YA KUKUSANYA MAONI YA KATIBA MPYA TANZANIA YAKOSOLEWA


Mkurugenzi mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dr. Helen Kijo-Bisimba
 Pamoja na kupongeza uteuzi wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema uteuzi huo unamapungufu.

Akitoa tamko jana kuhusu tume hiyo Mkurugenzi wa  LHRC Dr Helen Kijo Bisimba amewaambia waandishi wa habari kuwa  kituo hicho kimeona kuna mapungufu makubwa mawili ambayo ni

i) Kuwemo kwa mbunge na mjumbe wa baraza la wawakilishi
ii) Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine mfano vijana
Amesmema kituo hakikubaliani kabisa na uteuzi wa wakilishi wa wananchi (Mbunge na Mjumbe wa Baraza la wawakilishi). Wajumbe hawa ni Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada mwakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Sababu kubwa za kutokukubaliana na uteuzi wa wajumbe hawa ni kuwa kwanza, hawa watashiriki kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (constituent assembly) kwa hiyo kuna ‘mgongano ulio dhahiri wa kimaslahi’. (kwa mujibu wa vifungu cha 6 na 22 (1) (a) na (b) vya sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba, 2011)

Pili wananchi wanaowawakilisha watanyimwa haki yao ya kuwakilishwa kwa kipindi chote cha miezi 18 mpaka ishirini ambacho tume itafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Tatu, kuna majina mengi ambayo mheshimiwa Rais alipelekewa yenye sifa za kutosha angeweza kuwateua. Kulimbikiza kazi nyingi kwa watu wale wale si afya kwa demokrasia.

Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine
Katika tume hii tumeona kuna uwakilishi finyu sana wa makundi kwa mfano wanawake wako 10 kati ya 32, yaani sawa na asilimia 27% tu! Tungetegemea asilimia 50% kwa 50% kwani Tanzania imesaini na kuridhia mkataba wa nyongeza wa maendeleo ya kijinsia kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol. Pia 3

Tanzania ina asilimia ya 51 ya idadi ya wanawake ambao miongoni mwao wengi wana utaalamu na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.

WITO
I) Tunapenda kutoa wito kwa serikali kuwa mchakato wa Katiba ni wa muhimu sana hautakiwi kuchukuliwa kwa wepesi. Mchakato huu unajenga mustakabali wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Hivyo katika maamuzi yote yanayochukuliwa, kuwe na jicho la HAKI ZA BINADAMU na utawala wa sheria.

II) Pia tunapenda kutoa wito kwa WANANCHI wote wa Tanzania, mijini na vijijini, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, TUSHIRIKI kwenye mchakato huu. Tunawasihi kuwa Tume ya Katiba itakapokuja kwenye maeneo yetu tuhudhurie mikutano yote na kutoa maoni yetu juu ya Katiba Mpya.

Wananchi katika makundi au mtu mmojamoja anaweza kupeleka maoni ya maandishi kwenye tume mara anuani itakapojulishwa kwa wananchi.

III) Mwisho tunatoa wito kwa tume kuhakikisha watu wote wanatoa maoni yao bila ubaguzi. Makundi yote ya jamii yafikiwe (Wanawake, wanaume, watu wenye ulemavu na watoto wenye umri wa kutoa maoni).
Tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya ya Tanzania  yenye wajumbei 32 (akiwemo mwenyekiti na makamu) iliapishwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete  April 13 mwaka huu.
Wajumbe hao ni Mwenyekiti wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa tume toka Tanzania Bara ni Prof. Mwesiga L. Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Nd. Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Nd. Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi, Nd. Humphrey Polepole, Nd. Yahya Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd. Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku. 2

Wajumbe wengine 15 ni kutoka Tanzania Zanzibar. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman Hamad, Nd. Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi, Nd. Nassor Khamis Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf Mshamba, Nd. Kibibi Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama Kombo Ahmed, Nd. Abubakar Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally Saleh.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.