MTANGAZAJI

MCHUNGAJI WA KIADVENTISTA NA SAKATA LA CRYPTO NCHINI KENYA


Mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Kenya  Mch.Paul Mwangi amejikuta kwenye mjadala wa umma kufuatia kusambaratika kwa jukwaa la uwekezaji wa fedha za kidijitali( cryptocurrency) na forex liitwalo Optcoin, ambalo lilikuwa likihusishwa na mchungaji huyo ambaye ni kiongozi mwandamizi wa kanisa hilo nchini Kenya. Tukio hilo limeacha maelfu ya Wakenya wakiripoti hasara za kifedha zinazokadiriwa kufikia mamilioni ya shilingi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Business Daily Africa, watumiaji wa Optcoin waligundua hivi karibuni kuwa tovuti ya jukwaa hilo ilikuwa imetoweka ghafla. Baadhi yao walielekezwa kwenye mfumo mpya uliowataka kulipa ada ya usajili ya angalau Shilingi za Kenya 24,000, wakidaiwa kuwa ni sharti la kurejesha fedha zao. Hata hivyo, wengi wanasema hawajaweza kutoa pesa zao tangu mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu licha ya kupewa ahadi mara kwa mara.

Baadhi ya wawekezaji walioathirika wamesema walitambulishwa kwa Optcoin na Paul Mwangi, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Konferensi ya Kati ya Kenya katika kanisa la Waadventista (CKC) na ambaye kwa sasa ni Katibu Mtendaji wa Unioni Konferensi ya Kenya Mashariki (EKUC). 

 Mwekezaji mmoja ameimbia Business Daily Africa kuwa aliwekeza zaidi ya shilingi  200,000 za Kenya kabla ya kupoteza ufikiaji wa akaunti yake. Malalamiko yanayofanana yameibuka kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo X, TikTok, na Facebook, huku baadhi ya watumiaji wakiitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuingilia kati kuhusu suala hilo.

Optcoin ilijitangaza kama jukwaa la uwekezaji likiahidi faida kubwa, kamisheni za rufaa na utoaji wa fedha wa haraka. Hata hivyo, halikuwahi kuweka wazi taarifa za umiliki, usajili wala anwani ya ofisi, hali inayofanana na mifumo mingine ya uwekezaji wa mtandaoni isiyodhibitiwa, ambayo mamlaka zimekuwa zikiionya mara kwa mara kwa wananchi kutojihusisha nayo.

Baada ya kuanguka kwa jukwaa hilo, Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Kenya limesema kuwa halihusiki na Optcoin, likisisitiza kuwa wachungaji au viongozi waliolitangaza walifanya hivyo kwa misingi binafsi, si kwa niaba ya kanisa. Kanisa pia limekumbusha kuwa lilishawahi kutoa mwongozo unaowaonya wahudumu dhidi ya kushiriki katika uwekezaji usio na maadili au usiodhibitiwa.

Katika video iliyosambaa mtandaoni, Mchungaji Mwangi amesema naye pia ni mhanga wa Optcoin, akidai kupoteza zaidi ya dola 735,000 za  Marekani, sawa na takribani shilingi milioni  94 za Kenya, na kushindwa kutoa fedha zake.

Awali, Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) ya  Kanisa hilo katika barua yake ya Novemba 6, 2025 ilikuwa imetoa onyo rasmi kwa viongozi wake, ikisisitiza kuwa hakuna mhudumu au mfanyakazi wa kanisa anayepaswa kushiriki au kutangaza shughuli za uwekezaji zisizo halali au za udanganyifu, huku ikionya kuwa hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa kwa watakaokiuka mwongozo huo.

Sakata la Optcoin linaibua tena wasiwasi mpana kuhusu mifumo ya uwekezaji wa kubahatisha nchini Kenya, hasa pale inapohusishwa na viongozi wanaoaminika. Vyombo vya habari nchini humo vinaendelea kufuatilia maendeleo ya sakata hili huku wakisubiri maelezo rasmi kutoka kwa mamlaka na uongozi wa kanisa.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.